Mchina ambaye gari lake lilianguka ndani ya bwawa amepatikana akiwa amefariki baada ya kutoweka kufuatia tukio hilo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Daily Guide, marehemu ambaye bado hajafahamika jina lake inasadikiwa alikuwa akifanya kazi ya uangalizi wa kampuni ya ujenzi wa barabara wilayani Kwahu, Ghana.
Akiwa kazini, inasemekana mwanamume huyo aliteleza ndani ya bwawa hilo na gari lake.
Kulingana na hayo, kikosi cha upekuzi kilitumwa kumtafuta lakini hakuweza kupatikana ingawa inaaminika alikuwa amenasa majini.
Wajumbe wa baraza la kimila katika eneo hilo wanasemekana kufanya baadhi ya matambiko ikiwa ni pamoja na kumwaga sadaka ambayo hatimaye ilisababisha kupatikana kwa mwili huo Jumapili asubuhi.
Mwili huo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Familia Takatifu ya Nkawkaw kwa uchunguzi zaidi.