Mahakama ya Malawi imempata na hatia raia wa Uchina kwa mashtaka mengi yakiwemo ulanguzi na kushirikisha watoto katika burudani.
Lu Ke, ambaye pia anajulikana kwa jina la Susu, amehukumiwa kifungo cha miezi 12 jela, ambacho tayari ametumikia akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Ameamriwa kuondoka nchini ndani ya siku saba na amezuiwa kurejea tena.
Alikamatwa mwaka jana kufuatia ripoti ya uchunguzi wa BBC Africa Eye.
Ripoti hiyo ilimuonyesha akiwarekodi watoto wa Malawi wakitengeneza video za salamu za kibinafsi, baadhi zikiwa na maudhui ya ubaguzi wa rangi.
Video hizo zilikuwa zikinunuliwa kwa hadi $70 (£55) kwenye mitandao ya kijamii ya Uchina na majukwaa ya intaneti.
Wakati habari za video zake za kuudhi zilipoibuka, alikimbilia nchi jirani ya Zambia huku mamlaka ya Malawi ikitoa kibali cha kukamatwa kwake.
Alikamatwa na kupatikana na hatia ya kuingia nchini humo kinyume cha sheria na kisha kurejeshwa nchini Malawi.
Alinyimwa dhamana na amekuwa chini ya ulinzi wa polisi hadi hukumu yake siku ya Alhamisi.
Alikabiliwa na mashtaka 14 dhidi yake, yakiwamo ya kununua watoto kwa ajili ya matumizi ya burudani, ulanguzi wa watoto, matumizi haramu ya mtandao na mila potofu ya kijamii.
Hata hivyo, Lu Ke alikanusha kutengeneza video za kudhalilisha.
Katika utetezi wake, mahakama iliambiwa tayari alikuwa amelipa kwacha ya Malawi 16m ($16,000; £12,500) kwa serikali ili kuwafidia waathiriwa wake na kwa shughuli za uwajibikaji katika kijamii.
Lu Ke alijitetea akisema ametengeneza video zake ili kueneza utamaduni wa Wachina kwa jamii ya eneo.