Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge: Mkutano wa Ikulu Uliendeshwa kwa Bunduki Tatu Kuwekwa Mezani

Ruto Mbunge: Mkutano wa Ikulu Uliendeshwa kwa Bunduki Tatu Kuwekwa Mezani

Fri, 5 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbunge wa Kimilili nchini Kenya, Didmus Barasa amedai kuwa Rais Uhuru Kenyatta aliendesha mkutano wa wabunge wa Jubilee huku bunduki tatu aina ya AK47 zikiwa mezani kwake.

Mbunge Barasa ambaye anafahamika kama mwanachama mtiifu wa kambi ya Urais ya Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto, maarufu kama ‘Tanga Tanga’ kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao amewatetea wabunge wenzake kwa ukimya wao kuhusu hali hiyo kwa madai kuwa mazingira yalikuwa hatarishi.

Barasa amedai kuwa Kenyatta ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo alikataa kusikiliza malalamiko ya kambi ya Tanga Tanga.

‘’Mkutano uliendeshwa huku bunduki tatu za AK47 zikiwa zimewekwa mezani, hata hivyo tulinyoosha mikono yetu ili kuongea lakini mwenyekiti hakujali kutupa nafasi’’, Barasa alisema.

Mbunge huyo mkosozi wa sera za Uhuru Kenyatta alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Profesa Makau Mutua ambaye aliwakosoa wanakambi wa Naibu Rais Ruto kwa kusema kuwa wamekaa kimya wakati ambao Rais Uhuru Kenyatta anawashambulia wanakambi wengine.

‘’Nilifikiri kuwa leo huko Ikulu, wabunge waasi wa Jubilee; Moses Kuria, Ndindi Nyoro, Alice Wahome, Didmus Barasa, Kimani Ichung'wa, na Kimani Ngunjiri wangekabiliana na Uhuru Kenyatta na kukomesha ukandamizaji wake katika Bunge. Midomo Tu!, Mutua alibeza kambi hiyo ya Ruto.

Ripoti zinasema kwamba Mkutano wa Rais Kenyatta na wabunge ulidumu kwa dakika 30 tu ambapo Mwanasheria Mkuu wa Kambi ya Wabunge walio wengi, Benjamin Washiali na Makamu wake Cecily Mbarire waliondolewa kwenye nafasi zao.

Nafasi hizo zilijazwa na mbunge wa Navahkholo Emannuel Wanga na Mbunge wa Imenti Kaskazini, Maoka More.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live