Nairobi, Kenya. Mahakama Kuu nchini Kenya, imeamuru mbunge wa upinzani nchini Kenya, Paul Ongili maarufu Babu Owino kuendelea kukaa rumade kwa siku saba zaidi.
Babu Owino ameshtakiwa kwa kosa la jaribio la kuua kwa kukusudia baada ya kumpiga kwa risasi DJ katika ukumbi wa muziki.
Jaji Francis Andayi leo Jumanne Januari 21 aliagiza mbunge huyo aendelee kukaa kizuizini kwa siku saba zaidi hadi ombi lake la kutaka kuachiwa kwa dhamana litakaposikilizwa.
Jaji Andayi alisema endapo mbunge huyo atapewa dhamana kwa sasa anaweza kuharibu uchunguzi kwa kuwarubuni mashahidi wa kesi hiyo.
Ijumaa iliyopita, mbunge Owino alikamatwa na polisi kwa tuhuma za kumpiga risasi DJ mmoja baada ya kutofautiana.
Mbunge huyo ambaye alilala polisi kwa siku mbili, Jumatatu iliyopita alipandishwa kizimmbani na kusomewa mashtaka ya jaribio la kuua kwa kukusudia.
Pia Soma
- Wanafunzi 5,672 kati ya 22,810 waanza kidato cha kwanza Mtwara
- Mahakama yahoji upelelezi kesi ya Magoti wa LHRC
- Mahakama yaonya upande wa mashtaka kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Magufuli
Inaelezwa kuwa DJ huyu kwa sasa anaendelea kupata matibabu katika hospitali moja mjini Nairobi baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondolea risasi iliyompata shingoni.
Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa na wengi katika mitandao ya kijamii nchini Kenya ambako wengi walionyesha kiu ya kujua hatma ya mbunge huyo.
Kesi ya Babu owino inawadia wakati ambao polisi imetangaza kutotoa tena ulinzi kwa viongozi wa Serikali ambao wanakabiliwa na kesi za uhalifu.