Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge EALA ataka Tanzania kuongoza usuluhishi Sudan

Nchi Za Kiafrika Zasuasua Mataifa Yakiwaondoa Raia Wao Sudan Mbunge EALA ataka Tanzania kuongoza usuluhishi Sudan

Tue, 25 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MBUNGE wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), James Millya ametaka Umoja wa Mataifa (UN) kuunda timu itakayosaidia kuondoa mgogoro nchini Sudan ikiongozwa na Tanzania yenye uzoefu katika utatuzi wa migogoro Afrika.

Millya anayeiwakilisha Tanzania katika EALA, alisema katika mazungumzo na HabariLEO Afrika Mashariki kuwa, njia madhubuti ya kuondoa mgogoro nchini humo ni pande hizo mbili kukutana katika meza ya mazungumzo.

Alitaka Umoja wa Afrika (AU) kuunda timu itakayosaidia kukaa na pande hizo na kufanya upatanishi akisisitiza timu hiyo kuhusisha Tanzania kwa kuwa ina historia nzuri katika utatuzi wa migogoro katika nchi mbalimbali barani Afrika.

Tanzania imekuwa ikishiriki na kuongoza juhudi za utatuzi wa migogoro katika nchi mbalimbali barani Afrika zikiwemo Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) hali iliyosaidia nchi hizo kuwa na amani.

Kwa mujibu wa Millya, hatua hizo hazina budi kuchukuliwa haraka kwa kuwa mgogoro huo hauathiri Sudan pekee, bali nchi zote za Afrika ambapo kwa Tanzania kumekuwa na athari za kiuchumi na kijamii.

“Kijamii tuna wanafunzi wengi wanaosoma Sudan na sasa wanatakiwa kurejea nchini hivyo kuvuruga utaratibu wote wa masomo yao, lakini pia nchi inafanya biashara na Sudan hivyo kulazimisha kusitishwa,” alisema.

Awali, EAC ilitaka kumalizwa haraka kwa mgogoro nchini Sudan kwa pande zinazohusika kukaa, kujadili na kumaliza tofauti zao. EAC ilieleza kusikitishwa na mzozo huo na kutaka kusitishwa mara moja kwa uhasama kati ya pande zinazohusika ili kuepusha kuendelea kupoteza maisha, majeraha na uharibifu wa mali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live