Mchungaji aliyefariki wiki iliyopita nchini Eritrea hawezi kuzikwa kwa sababu hakuwa wa dini inayotambulika na serikali, vyanzo vya karibu vya familia yake vimeiambia BBC.
Makanisa ya Orthodox, katoliki na Kiinjili la Kilutheri, pamoja na Waislamu wa Sunni ndio dini pekee zinazokubaliwa rasmi nchini humo.
Wafuasi wa dini nyingine huwa wanamatwa, wanateswa na kutengwa na makanisa yote ya kiinjili yalipigwa marufuku tangu Mei 2002.
Mchungaji Tesfay Siyum, ambaye alifariki siku 11 zilizopita, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa kanisa la kiinjili la Meserete Kristos huko Eritrea, mchungaji ambaye sasa anaishi Ethiopia aliambia BBC.
Alikuwa gerezani kwa sababu ya imani yake kwa zaidi ya miaka 10 na aliachiliwa huru miezi miwili iliyopita kabla ya kufariki nyumbani kwake katika mji mkuu wa Asmara.
Kundi la kutetea uhuru wa kidini la Open Doors Canada lililaumu "urasimu" kwa matatizo ya kupata kibali cha mazishi ya Mchungaji Tesfay.
Familia yake imenyimwa ruhusa ya kumzika katika makaburi ya umma huko Asmara na katika makaburi katika kijiji alikotokea. Ndugu zake ikiwa ni pamoja na mkewe na binti yake wanaripotiwa kuwa katika msongo mkubwa wa mawazo.
Mazishi nchini Eritrea yanapaswa kufanyika haraka iwezekanavyo. Hatahivyo, Waziri wa habari hajajibu ombi la BBC la kutoa maoni yake kuhusu suala hilo.