Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawaziri EAC wateua watendaji EALA, EAHRC

3b7f97b26f1df4b00efafd478329c1bc.jpeg Irene Kisaka Mtanzania aliyeteuliwa kushika Kurugenzi EAC

Tue, 19 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki limefanya uteuzi wa watendaji wa kushika nafasi zilizo wazi katika mashirika na taasisi zake mbalimbali.

Miongoni mwa walioteuliwa ni Alex Obatre kuwa Katibu wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Christine Wekesa kuwa Naibu Msajili katika Mahakama ya Afrika Mashariki na John Njoroge kuwa Naibu Katibu wa EALA. Aidha, baraza hilo limepitisha makadirio ya bajeti ya Dola za Marekani milioni 91 ili kuwezesha mashirika na taasisi za EAC kutekeleza majukumu yake mwaka wa fedha 2022/2023 na kupeleka makadirio hayo EALA ili kuidhinishwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sekretarieti ya EAC, katika Mkutano Maalumu wa 47 uliofanyika Aprili 4 hadi 6, mwaka huu ukiongozwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri wa EAC na Maendeleo ya Kikanda wa Kenya, Betty Maina, watu 35 wenye sifa waliteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika mashirika na taasisi za EAC.

Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu wa EAC, Dk Peter Mathuki, Naibu Waziri (Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) wa Tanzania, Deogratius Ndejembi na Waziri wa Masuala ya EAC wa Burundi, Balozi Ezechiel Nibigira.

Wengine ni Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Rwanda, Dk Emmanuel Ugirashebuja, Waziri wa Masuala ya EAC wa Sudan Kusini, Deng Kuol na Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu na Waziri wa Masuala ya EAC wa Uganda, Rebecca Kadaga.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wengine walioteuliwa katika nafasi mbalimbali za taasisi na mashirika ya EAC ni Irene Isaka kuwa Mkurugenzi wa Sekta za Jamii, Arthemon Ndizeye kuwa Mkurugenzi wa Forodha, Aime Uwase kuwa Mkurugenzi wa Mipango na Julius Mbati kuwa Ofisa Uhusiano wa Polisi.

Katika taasisi za EAC, uteuzi mkubwa ni pamoja na Dk Felix Kayigamba kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Utafiti wa Afya ya Afrika Mashariki (EAHRC), Dk Masende Bwire kuwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) na Dk Sylvance Okoth anayeshika wadhifa kama huo katika Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika Mashariki (Easteco).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live