Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakili waruhusiwa kuonana na Bobi Wine kizuizini

C4375513121051535800b1f92432957e Mawakili waruhusiwa kuonana na Bobi Wine kizuizini

Fri, 22 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

Hatimaye jeshi la Polisi nchini Uganda na UPDF limewaruhusu wanasheria wa aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais Robert Kyagulanyi maarufu ‘Bobi Wine’ kumtembelea nyumbani kwake Magere anapozuiliwa na vikosi hivyo kwa zaidi ya wiki moja.

Hii ni baada ya Mahakama Kuu jana kutoa maamuzi ya ombi la Kyagulanyi na mkewe la kuondolewa kwa vikosi vya jeshi na polisi nyumbani kwake.

Mawakili hao waliruhusiwa kumuona baada ya kukaguliwa kwenye kizuizi cha jeshi kilichowekwa karibu na nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa mmoja wa mawakili wa mwanasiasa huyo, Asumani Basalirwa, aliyezungumza na BBC kwa njia ya simu amesema iliwachukua muda wa saa kadhaa kuwashawishi wakuu wa jeshi la UPDF na polisi kuweza kumuona mteja wao.

Mwanasheria Basalirwa ameeleza kuwa wamemkuta Bobi Wine akiwa na upungufu wa chakula kutokana na kumzuia kutotoka nje na pia kuwazuia watu kuingia nyumbani kwake ambao wangemletea chakula lakini hali yake kiafya sio mbaya.

“Afya yake ni nzuri, hakuna kitu chochote lakini yeye anataka kitu kimoja tu nacho ni haki yake, anataka apewe uhuru kutoka kwake nyumbani kwenda kufanya kazi yake kisha kurudi nyumbani,” amesema Basalirwa.

Akizungumzia mteja wake kuwekwa kizuizini Mwanasheria huyo amesema, “Walisema wao wako na intelijensia yao inayowaarifu kuwa Bobi Wine anafanya maandalizi ya kufanya vurugu na kuwaambia raia waandamane barabarani.”

Hii sio mara ya kwanza kwa jeshi la UPDF na polisi kuwazuia viongozi wa upinzani nyumbani kwao baada ya uchaguzi, Dk. Kiiza Besigye baada ya uchaguzi wa mwaka 2016 alizuiwa nyumbani kwake Kasangati kwa zaidi ya miezi mitatu hadi Rais Yoweri Museveni alipoapishwa.

Mahakama Kuu Uganda wiki ijayo Januari 25, itatoa uamuzi wa Bobi Wine na Mkewe Babra Itungo ambao wameomba mahakama kuwaondoa wanajeshi na polisi nyumbani kwake na kupewa uhuru wao wa kikatiba.

Chanzo: habarileo.co.tz