Rais wa Tunisia, Kais Saied amemfukuza kazi Waziri wa Nishati, Naila Nouira Al-Kenji ikiwa ni mara ya pili kwa afisa wa serikali kufutwa kazi ndani ya mwezi mmoja, ambapo awali Waziri wa Mambo ya Ndani, Tawfiq Charafeddine alitumbuliwa.
Taarifa ya Ofisi ya Rais, haikuweka wazi sababu za kufukuzwa kazi kwa Al-Kenji, na hata serikali ya Tunisia pia haijalizungumzia.
Hata hivyo, hatua hiyo huenda ikahusishwa na mzozo wa kisiasa na kiuchumi unaoendelea nchini humo hali iliyopelekea kuondolewa kwa Waziri huyo.
Tunisia, imekuwa ikikabiliwa na ghasia za kisiasa na kijamii tangu yalipofanyika mapinduzi ya mwaka 2011, na janga la Uviko-19 lililozidisha changamoto za kiuchumi.