Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauaji ya Kware Kenya: Mshukiwa adai aliteswa ili kukiri mauaji

Kenya Kwazidi Kuchafuka,vurugu Zaibuka Uwanja Wa Kamukunji.png Mauaji ya Kware Kenya: Mshukiwa adai aliteswa ili kukiri mauaji

Thu, 18 Jul 2024 Chanzo: Bbc

Collins Jumaisi Khalusha, anayetuhumiwa kuwaua takriban wanawake 42 na kuikatakata miili yao kabla ya kuwatupa kwenye machimbo ya mawe eneo la Kware, mjini Nairobi, amedai ukatili wa polisi kufuatia kukamatwa kwake siku ya Jumatatu.

Khalusha, kupitia kwa wakili wake John Maina Ndegwa, amedai kuteswa hadi kukiri kuwa aliwaua wanawake hao, huku akiiomba mahakama kumpatia huduma ya matibabu.

"Mteja wangu, akiwa amekaa pale, anahitaji matibabu ya haraka ... kwa sababu katika kipindi alichowekwa kizuizini, alinyanyaswa, kuteswa na kulazimishwa kukiri kwamba aliwaua watu 42 jambo ambalo ni la kuchekesha. ” alidai Ndegwa mbele ya Mahakama ya Sheria ya Makadara.

"Mteja wangu amefanyiwa ukatili wa kutisha ili aweze kukiri masuala ambayo si ya kawaida kwake. Ninaomba kwamba mahakama ielekeze uangalizi wa haraka wa matibabu hata wanapofanya uchunguzi wao''.

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) hata hivyo ilipuuzilia mbali madai hayo ya unyanyasaji, ikibaini kuwa ni afisa mmoja tu wa polisi aliyepewa mshukiwa kurekodi taarifa yake.

DCI ilitaka Khalusha azuiliwe kwa siku 30 hadi kukamilika kwa uchunguzi wa mauaji hayo, akisema iwapo ataachiliwa kuna uwezekano wa kuendelea na shughuli za uhalifu.

Shirika la upelelezi pia liliiambia mahakama kwamba wanahitaji muda zaidi wa kuwatafuta mashahidi na familia za wahasiriwa ambao wametawanyika kote nchini, na kwamba watahitaji pia kuchukua sampuli za DNA, utambulisho, na pia kumfanyia mshukiwa uchunguzi wa kiakili.

Upande wa mashtaka hata hivyo ulipinga hilo, badala yake uliitaka mahakama kuwapa polisi siku 14 pekee kumzuilia mshukiwa huku uchunguzi ukiendelea.

Hakimu Mkuu Irene Gichobi hata hivyo aliruhusu DCI kumzuilia mshukiwa katika kituo chochote cha polisi kwa siku 30 ilizoomba ili kukamilisha uchunguzi.

Chanzo: Bbc