Kamanda wa jeshi la Uganda – UPDF, Meja Generali Dick Olum amesema operesheni ya kuwaokoa wanafunzi waliotekwa nyara imeanza, huku akisema wauwaji kabla ya kutekeleza shambulio hilo walikaa Uganda kwa siku mbili. Meja Generali Olum ameyasema hayo wakati akihutubia wakazi wa mji wa Kasese magharibi mwa Uganda, baada ya tukio la kuuawa kwa wanafunzi 41 na wengine kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi.
Amesema, tayari wametuma ndege za kuwakoa wanafunzi waliochukuliwa baada ya tukio la uasi linaloshukiwa kufanywa na kundi la ADF huku akidai kuwa baadhi ya wanafunzi, haswa wavulana waliuawa huku wasichana wakikatwakatwa mapanga na wengine kuchukuliwa mateka.
‘’Walikuja hapa wakalala siku mbili, walitaka kuchoma magari wakaona magari ya jeshi wakarudi kwenye shule, sasa hivi tumetuma ndege kila sehemu inaenda kuwatafuta, tunataka kuokoa wale waliowateka,’’ amesema Meja Generali Olum Aidha ameongeza kuwa, “vijana walijaribu sana kupigana lakini walihakikisha wamechoma magodoro yao, nguvu ikawashinda, kwa wasichana walikuta mlango wazi, ndio wakaua na kukatakata.”