Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matukio ya ugaidi yafanya Rais kuomba msaada

Nyusi.png Rais wa Msumbiji Filipe Jacinto Nyusi

Wed, 4 Aug 2021 Chanzo: Nipashe

Rais wa Msumbiji Filipe Jacinto Nyusi anayetishiwa na waasi ameziomba Ulaya na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kusini mwa Afrika (SADC) kuokoa Cabo Delgado.

Hayo yanajiri baada ya mgogoro mdogo wa ndani nchini Msumbiji kuwa mkubwa na janga la kimataifa kikihitaji ushirikiano wa mataifa mbalimbali.

Magaidi wanaishambulia Msumbiji kwenye jimbo la Cabo Delgado, lililo mpakani mwa Tanzania mkoani Ruvuma. Rais wa nchi hiyo Filipe Jacinto Nyusi, akiwa kiongozi wa awamu ya nne ya taifa hilo, ndiye anayepambana na changamoto hiyo ambayo imekuwa pasua kichwa kwa eneo zima la Kusini mwa Afrika.

Nyusi aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kusini mwa Afrika (SADC) kuanzia Agosti 2020, ameomba msaada kukabili magaidi hao.

Tangu alipoingia madarakani Rais Nyusi, amekuwa mtetezi mkuu wa amani na kuimarisha usalama na amesaini mikataba mingi na makubaliano ya kuwa na amani baina yake na wapinzani wake wakuu chama cha RENAMO.

Nyusi aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi mwaka 2008 hadi 2014 wakati huo nchi hiyo ikiongozwa na Rais Armando Guebuza. Ilipofika 2014 alichaguliwa kuwa Rais kadhalika 2019 alipata tena ushindi na kuendelea kuliongoza taifa hilo.

Nyusi ameona kuwa hali ya Msumbiji si shwari na sasa ameomba msaada wa kimataifa kukabiliana na waasi wanaoendesha shughuli zao katika Jimbo la Cabo Delgado.

Mkakati wake wa kufurumusha makundi ya waasi ambayo yanaichachafya Cabo Delgado, jimbo lenye eneo kubwa zaidi nchini Msumbiji upande wa kaskazini, umeanza kuungwa mkono. Nchi za Ulaya na Marekani zimeonyesha nia ya kusaidia kumaliza uasi katika eneo hilo lenye utajiri wa gesi.

Vyombo vya habari vya kimataifa vinasema kuwa tayari Ureno imepeleka platuni mbili na Ufaransa kikosi kimoja wote wakijiandaa kuisaida Msumbiji kukabili uasi huo.

Marekani ambayo ilikuwa inangojewa zaidi kutoa jibu kuhusu suala hilo kwani tayari inakamilisha kuondoa vikosi vyake nchini Afghanistan ili kutoa msaada wa mashambulizi ya anga na kuzuia kutekwa nchi yote Taliban, imesema itapeleka wataalamu wa kufundisha vikosi vya jeshi la Msumbiji.

Siyo jambo la kushangaza kuwa Ufaransa inaongoza katika suala hilo kwani kampuni yake ya mafuta ya TOTAL ina mradi mkubwa wa kuzalisha gesi asilia (liquefied naturall gas) ambao sasa umefikia hatua kubwa na ni wa uwekezaji mkubwa.

Mjadala uliosikika katika vyombo vya habari vya kimataifa ni kama mfungamano huo wa kuisaidia Msumbiji utafaulu, kwani katika nchi nyingi uasi kama huo umekuwa ukisambaa na kuwa ni tatizo la kudumu, lililoota mizizi.

Ila ni lazima kukiri kuwa siyo kila mahali magaidi wameweza kukamata eneo na kumiliki, kwani kwa sehemu kubwa inategemea mizizi waliyonayo katika eneo husika, na hapo siyo kila mchambuzi wa habari au mshauri wa mamho ya nje anaweza kusema kwa uhakika nini kinahusika Msumbiji.

Ni tatizo mojawapo lililokwamisha nchi za Jumuia ya Maendeleo Kusini ya Afrika (SADC) kupanga mkakati wa kuingilia kati, wakihofia vita kubwa na hata kuisambaza katika nchi wanachama.

Moja ya maeneo ambayo yanalinganishwa na tatizo la Cabo Delgado ni Somalia, hasa kwa vile kundi hilo linajitambulisha kiitikadi na Al Shabaab, lililochipuka kutoka Al Qaeda na kimsingi ni moja ya matawi yake.

Tofauti ni kuwa kuna mparaganyiko wa kiitikadi na kisiasa nchini Somalia ambao unakuwa nguzo ya kundi hilo kujijenga ndani ya nchi, kwani halihitaji kutumia nguvu nyingi ili watu wawatii, kwa mfano juhudi zinazotumiwa na makundi ya kigaidi katika nchi za Afrika ‘magharibi ya Somalia.’ Halafu kundi la Msumbiji halina uwanja mpana kujificha na kuendeleza operesheni, kama Al Shabaab.

Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, alieleza miezi michache iliyopita kuwa kundi hilo ni lile lile lililoanza machafuko maeneo ya Mkoa wa Pwani na Lindi, likafurumishwa ndipo likahamisha maskani na kutua Msumbiji.

Ukiangalia maeneo hayo yanafanana, yana wakazi wanaoendana kwa lugha au utamaduni na dukuduku za hapa na pale dhidi ya serikali, kwa mfano ‘kuna utajiri wa mafuta lakini wananchi ni maskini,’ na wakati mmoja baadhi ya wanaoyapuuza makundi kama hayo wakasema walichukizwa na kukataliwa kukata mikoko maeneo ya bonde la mto Rufiji.

Kwa hasira hiyo walianzisha vita, walipue nchi. Suala la gesi hapa nchini lilileta chokochoko kwa mfano mwaka 2013 kukatokea maandamano mjini Mtwara, kundi la watu limebeba mabango kuhusu gesi, baadhi wakatoa dhihaka, ‘shemeji gesi haitoki,’ ikabidi Rais Jakaya Kikwete atoe tadhadhari, ‘nitawapelekea vita.’ Kungekuwa na mparaganyiko zaidi nchini wangeweza kujikita katika maeneo ya mbuga za mikoa hii ya Pwani, na mwelekeo ungekuwa kuzingira mitambo ya gesi kama wanavyofanya Msumbiji.

Ila tatizo linabaki pale pale, lile aliloainisha Waziri wa Mambo ya Nje, Liberata Mulamula hivi karibuni, Kinacholeta picha ya matumaini kiasi fulani ni kuwa licha ya kuwa dola Msumbiji limejikita zaidi maeneo ya kusini na mbuga za kaskazini ya nchi zina uhaba wa uwepo halisi wa serikali, serikali haina mparaganyiko wa kisiasa kuzuia kusonga mbele, endapo kunakuwapo hali bora zaidi ya uwezeshaji, kujenga ari miongoni mwa wapiganaji na makamanda kuwa mapambano hayo yanaweza kufikia tamati hitajika katika muda mfupi kiasi.

Tumaini pekee ni kuwa hasa kinachotakiwa ni kudhibiti nyendo za magaidi na ngome zao eneo la pwani (kwa mfano mji wa Pemba ambao una bandari), halafu kufuatilia njia za panya na maskani porini, kwa upana wa jimbo hilo lote.

Haitakuwa kazi ndogo kwani ni kama kupekua eneo lote la mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ili kufurumisha magaidi, lakini endapo hawawezi kuhamia kwa muda maeneo mengine na kurudi tena baadaye, wanaweza kukomeshwa.

Chanzo: Nipashe