Tume ya Umoja wa Afrika imekuwa muhanga wa uhalifu wa mtandaoni baada ya matapeli kutumia akili bandia ili kumuiga mkuu wa tume hiyo Moussa Faki na kuilenga miji mikuu ya nchi za Ulaya.
Huu unaweza kuwa upungufu wa kwanza wa kidiplomasia kwa teknolojia mpya.
Moussa Faki ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Sekretarieti ya Umoja wa Afrika mara kwa mara huwaandikia viongozi wa kimataifa wakati wowote anapohitaji kufanya mawasiliano.
Barua kama hiyo inajulikana rasmi kama "note verbale" (ujumbe wa maandishi) ni utaratibu wa kawaida wa kuratibu mikutano kati ya uongozi wa Umoja wa Afrika na wawakilishi wa nchi nyingine au mashirika ya kimataifa, lakini matapeli walitengeza sauti yake na kupiga simu kadhaa za video katika miji mikuu ya Ulaya, wakilenga kupanga mikutano.
Bado haijabainika matapeli hao walikuwa na nia gani, lakini taarifa ya AU ilisema barua pepe zao ni za uwongo, jambo linaloashiria kwamba wanaweza kuwa na nia ya kuiba vitambulisho vya kidijitali ili kupata ufikiaji habari za siri.
Deep fakes, teknolojia iliyotumiwa na wahalifu wa mtandao, zinazidi kuwa maarufu na mara nyingine hutumiwa na vyombo fulani kusambaza taarifa potofu na propaganda.
Teknolojia hizo zinahusisha matumizi ya akili bandia kutengeneza picha, sauti na sifa za mtu katika video inayoonesha mtu akifanya au kusema kitu ambacho hajawahi kufanya au kusema.