Mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan yamesema kuwa, yamejadiliana njia za kuweza kufikisha misaada ya dharura ya kibinadamu na kuikoa Khartoum, mji mkuu wa Sudan kutokana na mgogoro mkubwa uliowakumba wakazi wa mji huo.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, juhudi hizo tayari zimeanza kiasi kwamba jana Ijumaa asubuhi, malori yaliyokuwa yamebeba tani 460 za vifaa kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) yalifika Jabal Awlia mjini Khartoum, ambalo ni moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mapigano mjini humo.
Juhudi za OCHA ndizo zilizowezesha msafara wa malora hayo kufika eneo hilo. Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ilishirikiana na wahusika wa mzozo wa Sudan ili kuhakikisha kuwa malori hayo yanafika salama katika eneo lililokusudiwa.
Wananchi wa kawaida, wanawake na watoto wadogo ndio wanaoteseka zaidi Sudan
Mashirika ya misaada ya kibinadamu yamesema kuwa, tangu mwishoni mwa mwezi Mei, shirika la WFP limesaidia zaidi ya watu 150,000 katika eneo kubwa la Khartoum. Shirika hilo linaendelea kuongeza misaada yake kwa watu wanaokimbia makazi yao kwenye mji mkuu huo wa Sudan na kuelekea majimbo jirani kama ya Kaskazini na Mto Nile.
Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa (OCHA) pia imesema kuwa, eneo la magharibi mwa Darfur nalo limeonekana kuwa na changamoto nyingi kwa sababu ya mapigano baina ya majenerali wa kijeshi yaliyoanza tarehe 15 Aprili mwaka huu.
Sehemu moja ya taarifa ya OCHA imesema: "Kwa mara nyingine, tunatoa mwito kwa pande zote kuruhusu miaada inafika salama kwa walengwa kwenye maeneo yote ya Sudan, yakiwemo maeneo ambayo ni magumu kufikiwa.