Shirika la ndege la kitaifa nchini Kenya Airways, limetishia kuchua hatua za kinidhamu dhidi ya marubani wake huku mgomo ukiingia siku ya tatu.
Shirika hilo linashikilia kuwa mgomo huo sio halali; msimamo unaoungwa mkono na maafisa wa serikali ambao wanasema hatua za marubani 400 ni sawa na uhujumu uchumi.
Shirika hilo la kitaifa linasema lilighairi safari 56 za ndege mwishoni mwa juma, huku abiria takriban 12,000 wakiathiriwa na mgomo huo.
Usafirishaji na uingizaji wa mizigo kama vile mazao mapya na bidhaa za dawa pia umeathirika.
Shirika hilo la ndege sasa linaonya kuwa dirisha la mazungumzo linafungwa, na marubani waliohusika katika mgomo huo wanaweza kuachishwa kazi au kuchukuliwa hatua za kisheria.
Wizara ya Leba, Jumapili, ilisema shirika la ndege liko huru kuchukua hatua zinazofaa za kisheria dhidi ya marubani wake.