Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alizungumza kwa nyakati tofauti na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Félix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame na kujadili hali tete na mzozo mbaya wa kibinadamu kwenye mpaka kati ya mataifa hayo mawili na kuzitaka pande zote mbili kuondoa wanajeshi kwenye maeneo ya mpakani.Marekani ilitaka nchi hizo kupunguza mvutano baina yao.
Rwanda na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo zinashutumiana kwa uungaji mkono wa makundi ya waasi.Ifwatayo ni taarifa ya mwandishi wa BBC Yves Bucyana akiwa nchini Rwanda.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amewataka viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda kuhimiza kusitishwa kwa mapigano baada ya kuzuka kwa mapigano ya waasi wanaopigana dhidi ya Kinshasa. Kwa mjibu wa wizara ya nchi za nje ya Marekani,Akielekea Japan kutoka kwa ziara yake ya hivi punde Mashariki ya Kati, Blinken alizungumza kwa njia ya simu kando na Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa DR Congo Felix Tshisekedi kuhusu "hali tete" kwenye mpaka wao, Wizara ya Mambo ya Nje ilisema.
Blinken "alitetea suluhu la kidiplomasia kwa mvutano kati ya nchi hizo mbili na akahimiza kila upande kuchukua hatua za kukomesha hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wanajeshi kwenye mpaka," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Matthew Miller alisema katika taarifa yake.
Hakuna maelezo Zaidi yaliyotolewa kuhusu mahojiano hayo ila Ofisi ya Rais wa Rwanda ilisema Rais Kagame alisisitiza uungaji mkono mkubwa wa Blinken kwa mipango inayoendelea ya kikanda inayolenga "kuleta amani na utulivu" kwa DR Congo na kanda.
Waasi wa M23, wanapigana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wamezidisha mashambulizi tangu mwezi uliopita, huku Umoja wa Mataifa ukiripoti kuwa watu wengine 200,000 wameyakimbia makazi yao.
Siku ya Jumatatu, ripoti zilisema mapigano makali yaliendelea, huku M23 wakichukua tena baadhi ya maeneo kilomita chache kutoka mji wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa DR Congo.
Blinken mwaka jana alitembelea nchi zote mbili. Aliunga mkono hadharani madai ya Kinshasa kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi.
Serikali ya Rwanda inakanusha madai hayo lakini imetaka kuchukuliwa hatua katika nchi hiyo jirani dhidi ya waasi wa kundi la FDLR wanaohusishwa na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda ambayo yaliua zaidi ya watu 800,000 kwa mjibu wa umoja wa mataifa.