Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Marekani yazilaumu Rwanda na M23 kwa shambulio baya kwenye kambi DRC

Marekani Yazilaumu Rwanda Na M23 Kwa Shambulio Baya Kwenye Kambi DRC Marekani yazilaumu Rwanda na M23 kwa shambulio baya kwenye kambi DRC

Sat, 4 May 2024 Chanzo: Bbc

Marekani imelilaumu jeshi la Rwanda na kundi la waasi la M23 kwa shambulio baya katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Takribani watu tisa, wakiwemo watoto saba, waliuawa katika shambulio kwenye kambi ya Mugunga katika mji wa mashariki wa Goma siku ya Ijumaa.

Jeshi la Congo na M23 walilaumiana kwa shambulio hilo.

Rwanda, ambayo inapakana na DR Congo, inashutumiwa vikali kwa kuunga mkono kundi la waasi, jambo ambalo inakanusha.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema shambulio hilo la Ijumaa lilitoka katika maeneo yanayoshikiliwa na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) na kundi la M23.

Msemaji huyo alisema Marekani "ina wasiwasi mkubwa kuhusu upanuzi wa hivi karibuni wa RDF na M23" mashariki mwa DR Congo na kuzitaka pande zote mbili "kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia wajibu unaotumika chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu".

"Ni muhimu kwamba mataifa yote yaheshimu mamlaka ya kila mmoja na uadilifu wa eneo na kuwawajibisha wahusika wote kwa ukiukaji wa haki za binadamu katika mzozo wa mashariki mwa DRC," waliongeza.

Picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha miili ikiwa imelala chini kwenye kambi hiyo siku ya Ijumaa.

Wakazi wengi walikuwa wamekimbilia huko kutoroka mapigano katika miji na vijiji vyao.

Lt Kanali Guillaume Njike Kaiko, msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika eneo hilo, alisema shambulio hilo limekuja kulipiza kisasi mashambulizi ya awali ya Wacongo dhidi ya maeneo ya jeshi la Rwanda.

Rais Felix Tshisekedi, ambaye amekaa wiki kadhaa nje ya nchi, atarejea mwishoni mwa juma hili.

Wanajeshi wa waasi na serikali wote wameshutumiwa katika miezi ya hivi karibuni kwa unyanyasaji dhidi ya raia wakati wanapigania udhibiti wa maeneo.

Shambulio la hivi karibuni limetokea siku chache baada ya wapiganaji wa M23 kudai kuwa wameuteka mji wa Rubaya, eneo ambalo ni kitovu cha uchimbaji madini ya Coltan inayotumika kutengenezea simu za mkononi na betri za magari yanayotumia umeme.

Wakati huo huo, mahakama ya kijeshi mjini Goma imewahukumu kifo wanajeshi wanane wa DR Congo kwa "kutoroka" na "uoga" wakati wa kupambana na vikosi vya waasi, M23, iliyoundwa kama chipukizi la kundi jingine la waasi, ilianza kufanya kazi mwaka 2012 ili kulinda watu wa kabila la Watutsi mashariki mwa DR Congo, ambao kwa muda mrefu walikuwa wakilalamikia mateso na ubaguzi.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa kundi hilo linaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, ambayo pia inaongozwa na Watutsi, jambo ambalo Kigali imekuwa ikikanusha.

Chanzo: Bbc