Marekani imetangaza vikwazo vya viza dhidi ya maafisa wa sasa au wa zamani wa Somalia wanaotuhumiwa kuhujumu michakato ya kidemokrasia.
Hatua hiyo inawadia wakati ambapo Marekani inasukuma kufanyika kwa uchaguzi wa kuaminika nchini Somalia - ambao umechelewa kwa muda mrefu.
Katika taarifa, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alisema vizuizi vya visa vinatumika kwa watu “ambao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya kutekeleza uchaguzi kwa wakati na wazi“.
Pia vinalenga maafisa ambao “wamewalenga waandishi wa habari na wanachama wa vyama vya upinzani kwa unyanyasaji, vitisho, kukamatwa na vurugu“.
Somalia imeahirisha uchaguzi tangu mamlaka ya Rais Mohamed Abdullahi Farmajo yalipokamilika Februari mwaka jana.
Uchaguzi wa wabunge usio wa moja kwa moja ulianza Novemba na ulitarajiwa kuhitimishwa ifikapo tarehe 24 Disemba lakini umekumbwa na ucheleweshaji kutokana na migogoro.
Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble na viongozi wa majimbo ya kanda walifikia makubaliano tarehe 9 Januari kukamilisha uchaguzi ifikapo Februari 25.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani inasema viongozi hao wa kisiasa wanapaswa kufuata ahadi zao za kukamilisha mchakato huo kufikia tarehe ya mwisho iliyowekwa.
Vikwazo hivyo vinafuatia onyo la mwezi uliopita dhidi ya kucheleweshwa zaidi kwa uchaguzi.