Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Marekani yafanya mazungumzo na Jeshi la Niger

Marekani Yafanya Mazungumzo Na Jeshi La Niger Marekani yafanya mazungumzo na Jeshi la Niger

Tue, 8 Aug 2023 Chanzo: Bbc

Afisa muandamizi wa Marekani amefanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi wa kijeshi wa Niger kufuatia mapinduzi ya mwezi uliopita.

Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Victoria Nuland alisema mazungumzo yalikuwa "ya wazi kabisa na kuna wakati yalikuwa magumu".

Washington imesema mapinduzi bado yanaweza kumalizwa kidiplomasia na Rais Mohamed Bazoum kurejeshwa, lakini wakati huo huo imesitisha kutoa misaada nchini humo.

Nchi za Afrika Magharibi zinatazamiwa kukutana siku ya Alhamisi kujadili mzozo huo.

Ecowas - jumuiya ya kibiashara ya mataifa 15 ya Afrika Magharibi - ilikuwa imetoa hadi Jumapili usiku kwa viongozi wa serikali ya mapinduzi ya Niger kujiuzulu na kumrejesha rais aliyechaguliwa.

Viongozi wa mapinduzi walijibu tishio hilo la hatua za kijeshi kutoka kwa umoja huo kwa kufunga anga ya Niger.

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka mji mkuu wa Niamey, Bi Nuland alisema kuwa, katika mazungumzo yaliyochukua zaidi ya saa mbili, Marekani itasaidia Niger "ikiwa watu wanaohusika watakuwa na nia ya kurejesha utaratibu wa kikatiba" .

Bi Nuland alisema amekutana na mkuu mpya wa jeshi, Brigedia Jenerali Moussa Salaou Barmou, lakini hajakutana na aliyejitangaza kuwa kiongozi mpya wa Niger, Jenerali Abdourahamane Tchiani, au na Rais aliyepinduliwa, Bw Bazoum.

Bw Bazoum anaendelea kuzuiliwa lakini amezungumza na maafisa wa Marekani hapo awali kwa njia ya simu.

Bi Nuland aligusia pia wasiwasi juu ya madai ya viongozi wa mapinduzi waliomba kundi la mamluki la Wagner la Urusi kusaidia kudumisha udhibiti wa nchi.

"Watu ambao wamechukua hatua hii hapa wanaelewa vyema hatari ya uhuru wao kama Wagner itaingia hapa," alisema.

Chanzo: Bbc
Related Articles: