Marekani imehitimisha kuwa wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea pamoja na waasi walifanya uhalifu wa kivita wakati wa vita vikali vilivyodumu kwa miaka miwili, kaskazini mwa Ethiopia.
Blinken, ambaye alisikika kuwa mwenye matumaini wakati akiwa nchini Ethiopia kuhusu uwezekano wa kupatikana amani baada ya muafaka wa Novemba 2, alitoa wito mkali wa uwajibikaji aliporejea Washington.
Akizungumza wakati akizindua ripoti ya kila mwaka ya Marekani kuhusu haki za Binaadamu, Blinken alisema vitendo vingi vilivyofanywa havikuwa vya kubahatisha au matokeo tu ya kivita. Vilipangwa na kufanywa makusudi.
"Baada ya wizara ya mambo ya kigeni kuchunguza kwa umakini sheria na ukweli, nimehitimisha kuwa vikosi vya Ulinzi wa Kitaifa vya Ethiopia, Vikosi vya Ulinzi wa Eritrea, vikosi vya TPLF na vikosi vya Amhara vilifanya uhalifu wa kivita wakati wa vita vya kaskazini mwa Ethiopia."
Blinken aliongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Kigeni pia iligundua kuwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu ulifanywa na vikosi vya Ethiopia, Eritrea na Amhara, ikiwemo mauaji na unyanyasaji wa kingono, ijapokuwa hakutaja TPLF.
Vikosi vya kikanda vya Amhara vilipigana Pamoja na serikali. Blinken alisema vilifanya kile alichokiita usafishaji wa kikabila kwa kuwahamisha kwa nguvu watu kutoka magharibi mwa Tigray. Amezihimiza serikali ya Ethiopia na serikali ya Eritrea Pamoja na TPLF kuwawajibisha wale waliohusika na ukatili huo.