Marekani na serikali ya Somalia Alhamisi walisaini mkataba wa usalama ambao waliueleza kama wa kujenga jeshi la Somalia linalofanya kazi kwa ufanisi, lenye uwezo wa kuchukua majukumu ya kiusalama na kupambana dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab.
Katika hafla iliyoongozwa na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud mjini Mogadishu, nchi hizo mbili zilisaini makubaliano ya awali kwa ajili ya ujenzi wa kambi tano za kijeshi kwa jeshi la taifa la Somalia.
Kulingana na taarifa ya shirika la habari la serikali ya Somalia, SONNA, kambi hizo zitakuwa za kikosi cha Danab, kitengo maalum cha jeshi kilichopewa mafunzo na Marekani.
“Ndani ya miezi kadhaa tunatarajia kufikia idadi ya wanajeshi 3,000 wa kikosi cha Danab kilichoundwa mwaka wa 2017. Kikosi hicho cha Danab kinaandaliwa pia kukabidhiwa majukumu mengi yanayohitaji kuimarisha jeshi, na tayari kimepewa jukumu la kuajiri na kutoa mafunzo,” alisema Molly Phee, waziri mdogo wa Marekani wa mambo ya nje anayehusika na masuala ya Afrika.
Phee, ambaye alikuwa kwenye hafla hiyo, alisema Marekani inaisidia Somalia ili jeshi lake liwashinde wanamgambo wa al-Shabab.