Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Marais wasifu kubadilishana uongozi kwa amani, utulivu

660ddeca8543e53d2c0189c7f1ef34b2 Marais wasifu kubadilishana uongozi kwa amani, utulivu

Tue, 17 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKUU wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanajivunia mabadiliko ya kidemokrasia ya uongozi katika nchi zilizofanya uchaguzi na kubadilisha madaraka kwa amani katika ukanda huo.

Wamesema hatua hiyo imedhihirisha kuwa SADC ni mfano wa kuigwa katika demokrasia si tu kwa Afrika, bali duniani kwa ujumla.

Nchi zilizofanya uchaguzi na kubadilishana madaraka kikatiba kwa amani ni Zambia (Agosti 2021), Shelisheli (Oktoba 2020) na Tanzania (Machi 2021).

Akizungumza katika Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC jana jijini Lilongwe, Malawi, Mwenyekiti wa SADC aliyemaliza muda wake, Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi alisema nchi za Tanzania, Shelisheli na Zambia zimeonesha uimara wa jumuiya hiyo na demokrasia ya kweli.

Nyusi katika mkutano huo alikabidhi kijiti cha uenyekiti wa SADC kwa Rais wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera. Dk Chakwera alisema kwenye mkutano huo kuwa, inahitajika nguvu ya pamoja kuendeleza demokrasia, amani na utulivu wa kikanda kwa maendeleo ya wananchi wa jumuiya hiyo.

Naye Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alijitambulisha kwa viongozi wenzake ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki mkutano huo baada ya kuapishwa kuwa Rais na akawaomba wampe ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.

“Ni heshima kubwa kwangu kupata fursa hii adhimu kuzungumza katika mkutano wa wakuu wa nchi na serikali wa SADC, ni mara ya kwanza kuzungumza kwa nafasi hii (Rais), lakini nimezungumza mara kadhaa pia nikiwa Makamu wa Rais na pia katika mkutano maalum wa wakuu wa nchi za SADC uliofanyika Juni, mwaka huu Maputo, Msumbiji,” alisema.

Rais Samia alitoa shukrani zake na za Watanzania kwa mshikamano ambao viongozi wa SADC waliipa Tanzania wakati taifa lilipopita katika wakati mgumu wa kifo cha Rais John Magufuli Machi, mwaka huu.

Rais wa visiwa vya Shelisheli, Wavel Ramkalawan aliyehutubia mkutano huo kwa njia ya mtandao, aliipa pole Tanzania kwa kuondokewa na Dk Magufuli na kumuelezea kuwa alikuwa kiongozi mwenye maono.

Rais Samia pia aliwapongeza marais waliochaguliwa hivi karibuni akiwemo Rais mteule wa Zambia, Hakainde Hichilema na kusema ushindi wake ni matokeo ya uchaguzi wa amani walioufanya wananchi wa Zambia na kuahidi ushirikiano wa Tanzania kwa nchi hiyo.

Pia Rais Samia alimpongeza Rais wa Shelisheli, Ramkalawan kwa kuchaguliwa Oktoba, mwaka jana kuongoza taifa hilo.

Aidha, alimpongeza Katibu Mtendaji wa SADC aliyemaliza muda wake, Dk Stergomena Tax kwamba uongozi wake uliiwakilisha vyema Tanzania.

Chanzo: www.habarileo.co.tz