UCHAGUZI Mkuu uliofanyika nchini Tanzania umeelezwa kukidhi vigezo kulingana na mwongozo wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hivyo viongozi wa nchi wanachama wamepongeza mafanikio hayo.
Timu ya watazamaji wa EAC imeeleza kuwa kulingana na vigezo vya uchaguzi, viliyoainishwa katika Mwongozo wa Uchaguzi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, uchaguzi wa Tanzania umekidhi vigezo vyote na ulikuwa huru na haki.
Viongozi mbalimbali wamempongeza Rais Mteule John Magufuli kwa kushinda tena kiti cha urais kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Dk Magufuli alipeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania tena nafasi hiyo kwa miaka mingine mitano, akiwa miongoni mwa wagombea 15.
Alishinda kwa kupata kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 ya kura halali. Miongoni mwa marais waliompongeza Magufuli ni Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye.
Kiongozi huyo alimpongeza Magufuli kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muhula wa pili na aliwapongeza Watanzania kwa kuamua hatma yao kwa amani na kuonesha ukomavu wa demokrasia.
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alimpongeza Dk Magufuli kwa kuchaguliwa tena, akisema kuchaguliwa tena kunaonesha upendo, uhakika na imani waliyonayo wananchi wa Tanzania kwa uongozi wake.
“Kwa niaba ya watu na Serikali ya Jamhuri ya Kenya na kwa niaba yangu mwenyewe, nakupongeza kaka yangu, Dk John Pombe Magufuli kwa ushindi wako na wa chama chako Chama Cha Mapinduzi; kuchaguliwa kwako tena kunaonesha upendo, heshima na kuvutiwa kwa Watanzania kwako na utawala wako, pia ni nafasi ya kuweza kutekeleza mipango uliyonayo kwa ustawi wa nchi yako,” alisema Rais Uhuru.
Aliongeza “Kenya tutaendelea kufanya kazi na utawala wako kwa faida ya watu wa nchi zote mbili, kwa ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa ustawi wa amani, utulivu na ukuaji wa Bara la Afrika.”
Alimhakikishia kuwa Kenya itaendelea kushirikiana naye. Kiongozi wa Timu ya Watazamaji ya EAC, Rais wa zamani wa Burundi, Sylvestre Ntibantunganya alisema uchaguzi huyo ulikuwa wa huru na wa haki.
Timu hiyo iliundwa na watazamaji 59 waliosambazwa kwenye mikoa 13 nchini. Timu pia ilifuatilia utangazaji wa matokeo ya awali ya uchaguzi, yaliyokuwa yanatolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na yale yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Ntibantunganya alisema timu hiyo ilitembelea vituo 160 vya kupigia kura na kubaini kuwa kwa kiwango kikubwa kazi ya uchaguzi, ilifanyika katika mazingira ya amani na utulivu.
Alisema pia vyama vilivyoshiriki katika uchaguzi na wagombea wao, waliendesha kampeni zao nchi nzima katika mazingira ya amani na utulivu na vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kulingana na matakwa ya sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi, hivyo uchaguzi uliendeshwa kwa uhuru, amani na utulivu.
“Uchaguzi uliandaliwa na kusimamiwa kwa weledi wa hali ya juu, timu inaipongeza tume kwa namna inavyoendelea kutoa matokeo kwa haraka kadri inavyoyapokea,” alisema Ntibantunganya.
Ntibantunganya aliviomba vyama hivyo, vitangulize maslahi ya Watanzania kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu.
Wakati wa kukabidhiwa cheti cha ushindi kwa Rais Mteule Dk Magufuli kwenye ofisi za Makao Makuu ya NEC jijini Dodoma, Ntibantunganya alipongeza Watanzania kwa uchaguzi wa amani na kuvipongeza vyama vilivyoshiriki kwenye uchaguzi huo kwa jitihada za kutunza amani na usalama