Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya mhubiri aliyenaswa adaiwa kuwatibu wagonjwa

Mapya Mhubiri Mapya mhubiri aliyenaswa adaiwa kuwatibu wagonjwa

Mon, 12 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanandoa wilayani Misungwi wanashikiliwa na polisi wakituhumiwa kuanzisha kanisa pasipo kibali na kuwaombea wagonjwa waliowazuia kwenda hospitali, huku wakiwatoza Sh30,000 kwa huduma hiyo.

Waliokamatwa ni William Masuma na Kabula Lushika, wakazi wa Kijiji cha Nyamayinza, Kata ya Gulumungu wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza, wanaodaiwa kuwazuia waumini zaidi ya 200 kwenda kutibiwa hospitalini.

Kijiji hicho kipo umbali wa kilomita takribani 150 kutoka ulipo mnara wa Samaki katikati ya Jiji la Mwanza.

Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Misungwi ilifika katika makazi ya wanandoa hao na kukuta ibada ikiendelea kwenye Kanisa la Lulembo ambalo muonekano wake unafanana na darasa.

Katika ukaguzi uliofanyika juzi, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paulo Chacha alibaini kuwapo wagonjwa zaidi ya 200 katika makazi yanayoundwa na nyumba zilizojengwa kwa tope na kuezekwa nyasi, huku zaidi ya 50 wakiwa mahututi wakishindwa kutembea.

Chacha alisema wanandoa hao wenye leseni ya kutoa huduma za tiba asili kwa zaidi ya miaka mitano wamekuwa wakiendesha ibada bila kibali. Bila kutaja idadi, mkuu huyo wa wilaya alisema ofisi yake imepokea taarifa ya kuwapo vifo vya watu katika makazi hayo.

Chacha aliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kubaini iwapo kuna wagonjwa walifariki dunia na kuzikwa katika eneo hilo.

“Watu wanakufa hapa ninyi hamna taarifa, yupo mama tunavyoongea hapa alijifungua watoto pacha kwenye kituo cha afya akaruhusiwa, alipofika nyumbani hali ikabadilika, badala arudishwe hospitalini akaletwa kulazwa hapa akafa. Yule mama ameacha watoto wachanga,” alisema Chacha.

“Hawa mnaowaona hapa zaidi ya 200 ni wagonjwa, hebu oneni kwa macho yenu. Wote tumeshuhudia wagonjwa wengi kwenye eneo hili ambalo lina mabanda zaidi ya 100, hawa mkiwaangalia kwa hali zao wanahitaji maombi au kupelekwa hospitalini wakapatiwe matibabu.

“Naelekeza polisi wafanye utafiti kubaini kama kuna makaburi hapa au hayapo. Inawezekana kuna ndugu zenu wanazikwa hapa hamna habari; kanisa hilo lisitumike tena kwa sababu hawana kibali cha kuendesha kanisa, kama wanahitaji kutoa huduma hiyo waombe kibali cha kufanya hivyo,” alisema.

Alipotafutwa na Mwananchi jana, Chacha alisema wagonjwa 14 kati ya 50 waliokuwa taabani wamehamishiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa ajili ya uangalizi maalumu, huku wengine wakiendelea na matibabu kwenye kituo cha afya cha Misasi wilayani humo.

Kauli ya mhubiri

Mhubiri Masuma kabla ya kupelekwa kituo cha polisi alidai kuwa, hakuna wagonjwa waliokufa katika eneo hilo kwa kuwazuia kwenda hospitali.

Alidai kuwa anatoa huduma ya maombi kwa wenye imani kwamba watapona kwa kuombewa.

Masuma alisema wito wa kufanya maombezi aliupata miaka 10 iliyopita baada ya kuugua ugonjwa usiofahamika na hakupona hospitalini, bali alipoombewa na mhubiri, ambaye pia alimweleza ana karama ya kuponya maradhi kwa kutumia maombi.

“Ninafanya maombi tu sitoi huduma ya matibabu hapa. Kuna magonjwa siwezi kuyatibu, mfano mtu akiletwa anaumwa ugonjwa wa kupungukiwa damu huwa namshauri aende hospitalini au kama ana malaria ninamshauri aende hospitalini.

“Nawapokea wagonjwa, nawapatia eneo wajenge nyumba wanayoweza kumudu kuishi na kuhusu fedha wanapofika wanatoa ka-hela kadogo kwa ajili ya huduma hiyo, nyingine wanatoa wakishapona. Kuhusu mtu kufa akiwa hapa sina taarifa,” alisema mhubiri huyo.

Baada ya mkuu wa wilaya kutangaza kusitisha huduma, baadhi ya wagonjwa waliruka sarakasi, huku wakiangua kilio wakidai hawako tayari kuona huduma hiyo inasitishwa. Maombi hayo hayakufua dafu, baada ya Polisi kuingilia kati na kuwachukua kwenye karandinga na kuwapeleka katika kituo cha afya cha Misasi.

Mkazi wa Mwamazengo wilayani hapa, Elizabeth Sanyenge aliyefuata huduma kijijini hapo alisema alifika Februari mwaka huu kwa maelekezo ya shangazi yake kwamba tatizo lake la muda mrefu la maumivu ya mgongo, kiuno na kifua litaponywa.

“Tukiwa hapa tunaambiwa ‘omba tu.’ Kuanzia asubuhi ni kuomba kisha tunarejea ndani, tunashukuru baadhi yetu wamejisikia vizuri wakaondoka,” alisema Elizabeth.

Mgonjwa mwingine, Petro Lunalika alisema, “nina miezi sita kwenye makazi haya nikisumbuliwa na tatizo la moyo. Tangu nimekuja hapa na kufanyiwa maombi sasa naendelea vizuri.

“Tulisikia taarifa huku kuna maombi mtu yeyote anayeugua analetwa hapa, tukamleta mjomba wangu eneo hili miezi mitatu akiwa haoni, sasa anaendelea vizuri wala sijawahi kusikia mtu yeyote amefariki dunia,” alisema Juma Emmanuel, mkazi wa Songile wilayani hapa.

Alisema wagonjwa wanaofika kutibiwa katika eneo hilo hupatiwa eneo kwa ajili ya kujenga makazi bila kujali yatakuwa na ubora au usalama.

Aprili 15 mwaka huu huko Kenya, Mchungaji wa Kanisa la Good News International, Paul Mackenzie alikamatwa na Polisi baada kudaiwa kuwaambia waumini takribani 600 wafunge ili wafe wakaonane na Yesu, huku zaidi 200 wakipoteza maisha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live