Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapinduzi ya kijeshi yalivyotikisa nchi za Afrika 2023

Kiongozi Wa Serikali Ya Gabon Akataa Kuchukua Mshahara Wa Rais Mapinduzi ya kijeshi yalivyotikisa nchi za Afrika 2023

Tue, 26 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika kipindi cha miaka minne (2020-2023) bara la Afrika limeshuhudia mapinduzi kadhaa ya kijeshi hasa katika nchi za ukanda wa magharibi mwa bara hilo.

Mapinduzi hayo yalifanyika Burkina Faso, Mali, Guinea, Niger na Gabon baada ya kipindi kirefu cha utulivu, ambao ulilisaidia bara la Afrika kuwa moja ya maeneo yaliyoshuhudia ukuaji wa kiuchumi na uwekezaji.

Kumekuwa na hisia mseto kuhusu hatua ya wanajeshi kuchukuwa mamlaka ya uongozi uliochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Wale wanaounga mkono hatua hiyo wanasema ndio njia pekee ya kukomesha ukoloni mambo leo na wale wanaopinga wakisema inatishia amani, utulivu na maendeleo ya Afrika.

Tunapoelekea kukamilisha mwaka 2023 tunaangazia matukio makuu yaliyofanya nchi za kanda ya Afrika magharibi kutawala vichwa vya habari.

Gabon

Mnamo Agosti 30, 2023 viongozi wa jeshi la nchi hiyo walitangaza kumweka kizuizini Rais Ali Bongo muda mfupi baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza mshindi rais huyo aliyekuwa akigombea muhula wa tatu madarakani.

Maofisa hao walijitokeza kwenye televisheni ya taifa na kutangaza kwamba wamechukuwa mamlaka, kufunga mipaka ya nchi hiyo na kuvunja taasisi zote za serikali

Raia wa Gabon walipiga kura Jumamosi ya Agost 26, 2023 kumchagua Rais, Wabunge pamoja na serikali za mitaa ambapo Ali Bongo alikuwa akigombea urais huku akimenyana na mpinzani wake Albert Ossa.

Upinzani ulidai uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu baada ya Bw Bongo kutangazwa kuwa amepata asilimia 64 ya kura zilizopigwa. Ushindi wa Bongo ungemfanya aendelee kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa tatu wa miaka saba kulingana na katiba

Kupinduliwa kwa Ali Bongo kulitamatisha uongozi wa família yake uliyodumu kwa zaidi ya miaka 50 madarakani ambapo baba yake pekee Omar Bongo Ondimba aliongoza kwa takriban miaka 42 kabala ya mwanaye kuchukuwa hatamu ya uongozi.

Ali Bongo aliingia madarakani mwaka 2009 baada ya kifo cha baba yake na kutawala kwa miaka 14 hadi uchaguzi uliofanyika Agosti 26 mwaka huu ambao ungemuweka madarakani hadi 2030.

Niger

Nchini Niger nako wanajeshi walifanya mapinduzi Julai 26, 2023 wakiongozwa na Jenerali Abdourahamane Tchiane.

Kuondolewa madarakani kwa Rais Mohamed Bazoum kuliitumbukiza Afrika Magharibi katika mgogoro wa kikanda baada ya nchi jirani za Mali na Burkina Faso ambazo pia zilifanya mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021 na 2022 mtawalio kuunga mkono hatua hiyo.

Tawala za kijeshi za nchi hizo zilionya kuwa uingiliaji wowote wa kijeshi dhidi ya viongozi wa mapinduzi ya Niger utachukuliwa kuwa "tangazo la vita" dhidi ya Burkina Faso na Mali.

Duru zinaarifu kuwa kilichochochea mapinduzi nchini Niger ni mipango ya Bazoum kutaka kufumua uongozi wa juu wa jeshi na kumng’oa Jenerali Tchiani kutoka katika wadhfa wake wa mkuu wa majeshi.

Hiyo ni alama tosha kuwa mapinduzi hayo wala hayakuwa na nia ya kuirejeshea Niger mamlaka yake kamili ya kujitawala ama kuwakwamua wananchi kutoka kwenye umasikini bali kulinda maslahi ya maafande wakuu wa jeshi.

Rais Bazoum aliapishwa kuwa kiongozi wa Niger tarehe 2 Aprili 2021, akimrithi Mahamadou Issoufou ambaye alikuwa ameongoza nchi hiyo kutoka 2011 hadi 2021.

Alikuwa mshirika wa karibu wa mataifa ya Magharibi na waangalizi wanaamini kuwa anazuiliwa nyumbani kwake katika mji mkuu wa Niamey. Utawala wa Bazoum umeshirikiana na nchi za Ulaya katika jitihada za kujaribu kudhibiti wimbi la wahamiaji katika Bahari ya Mediterania.

Alikubali kurejesha mamia ya wahamiaji kutoka nchini Libya na pia kukabiliana na walanguzi wa binadamu katika vituo muhimu vya usafiri kati ya Afrika Magharibi na Kaskazini. Baada ya utawala wa Bazoum kutimuliwa madarakani, mpango huo sasa huenda ukasambaratika.

Guinea Mapinduzi ya kushtukiza ya kijeshi nchini Guinea yalimaliza hatamu ya uongozi wa Rais Alpha Conde uliokumbwa na utata, chini ya mwaka mmoja baada ya kushinda muhula wa tatu uliogubikwa na maandamano mabaya na ukandamizaji mkali dhidi ya upinzani katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika.

Conde, mwenye umri wa miaka 83, alizuiliwa na wanajeshi wa kikosi maalum (GFS) mnamo 5 Septemba 2021, saa kadhaa baada ya ufyatulianaji wa risasi kuripotiwa karibu na makazi ya rais mjini Conakry.

Wakosoaji walihoji kuwa kiongozi huyo alifanya kazi kwa miongo kadhaa kurejesha demokrasia, lakini mara tu alipoingia madarakani, aliidhoofisha.

Kamanda wa GFS Kanali Mahamady Doumbouya alithibitisha kuchukua serikali kupitia Runinga ya serikali na kuahidi kusimamia mabadiliko ya serikali kwa njia ya amani.

Burkina Faso Chini ya miezi mitano baada ya wanajeshi kuonekana kwenye televisheni ya taifa nchini Guinea wakitangaza kuwa wamemuondoa madarakani Rais Alpha Condé, tukio hilo lilijirudia tena nchini Burkina Faso, huku jeshi likitangaza kupinduliwa kwa mkuu wa nchi Roch Kaboré.

Chanzo cha uasi wa jeshi la Burkina Faso, kama ilivyokuwa nchini Mali, ni mzozo wa usalama unaosababishwa na wanamgambo wenye itikadi kali ambao ulisababisha madhara makubwa.

Ripoti zisizokoma za mashambulizi ya wanamgambo zilichochea ghadhabu ya umma huku hisia za chuki zikiibuka miongoni mwa wanajeshi waliohisi wanatumwa nje, wakiwa na silaha nyepesi mno, na kulipwa ujira mdogo au hata kupatiwa mlo kidogo, kuendeleza mapambano dhidi ya makundi ya wanamgambo.

Mali Mali imeshuhudia mapinduzi mawili ya kijeshi ndani ya mwaka mmoja (miezi tisa) baada ya Kanali Assimi Goïta kumuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keïta mwezi Agosti mwaka 2020 na rais wa mpito, Bah Ndaw, mwezi Mei 2021.

Raia wa Mali walikaribisha kutimuliwa kwa Bw Keita - lakini utawala wa wanajeshi katika serikali hiyo ya mpito ulilaumiwa kutokana na kasi ndogo ya utekelezaji wa mageuzi yaliyoahidiwa baada ya mapinduzi ya kwanza.

Baada ya kuchukua uongozi Kanali Assimi Goïta alisema Rais Bah Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane walishindwa kutekeleza majukumu yao na walikuwa na njama ya kuhujumu mchakato wa mpito nchini humo kwa kukiuka vifungu vya katiba viliyounda serikali mpito.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live