Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinapigana na Jeshi la Sudan nje ya mji wa Wad Madani katika Jimbo la Al-Jazira (katikati mwa Sudan) na kwamba mapigano hayo yamelazimisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao na kuelekea maeneo salama.
Likinukuu watu walioshuhudia, shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa Jeshi la Sudan, ambalo linadhibiti eneo la Wad Madani tangu mapigano yalipoanza katikati ya mwezi wa Aprili, lilifanya mashambulizi ya anga mashariki mwa mji huo ili kuzima shambulio lililoanzishwa na wapiganaji wa RSF siku ya Ijumaa iliyopita.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, Kikosi cha Msaada wa Haraka, kikiongozwa na Mohamed Hamdan Hemedti, kimejibu mashambulio hayo ya anga kwa mizinga, na kwamba wapiganaji wake wameonekana wakisonga mbele kuelekea eneo ambalo mapigano yalikuwa yanaendelea.
Picha zilizochukuliwa eneo hilo pia zimeonyesha nguzo za moshi ukipanda kutoka viunga vya mji huo.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu imethibitisha kwamba mapigano yalizuka Ijumaa asubuhi katika vitongoji vya Wad Madani, ambavyo vimewapa hifadhi zaidi ya watu 86,000 kati ya wakimbizi 500,000 waliokimbilia Jimbo la Al-Jazira.
Mamilioni ya raia wamekimbia makazi yao Sudan kutokana na vita Video ilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha umati wa watu wakikusanya mali zao na kuondoka Wad Madani kwa miguu.
Wakati huo huo Muungano wa Madaktari wa Sudan umeonya - katika taarifa yake- kwamba hospitali za eneo hilo, ambazo zimekuwa vituo vya masuala ya kibinadamu na matibabu, zimekuwa tupu, na huenda zikalazimika kufunga milango.
Juhudi za upatanishi wa kuhitimisha mapigano ya wenyewe kwa wenye nchini Sudan zimeambulia patupu hadi sasa huku kila mmoja kati ya wababe wa vita hivyo, Abdel Fattah Al-Burhan na Jenerali muasi, Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), akiendelea kung'ang'ania misimamo yake.
Siku chache zilizopita, Mkuu wa Baraza la Utawala nchini Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan, alitangaza kwamba hatakuwa tayari kukutana na Jenerali muasi, Mohamed Hamdan Dagalo ila baada ya kukubali usitishaji vita wa kudumu nchini humo, na kuondoka kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) mjini Khartoum.