Mapigano yameendelea kuripotiwa katika eneo lenye utulivu la Amhara nchini Ethiopia kati ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo wa eneo hilo huku mji wa kihistoria wa Gondar ukishuhudia mapigano makali mijini siku ya Jumapili.
Wanamgambo wa eneo hilo wanaojulikana kwa jina la Fano waliingia katika jiji hilo ambalo ni mojawapo ya miji mikubwa zaidi katika eneo hilo na kusababisha makabiliano makali na jeshi.
Taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa Facebook wa Jeshi la Ulinzi la Taifa la Ethiopia (ENDF) ilithibitisha mapigano hayo na kuongeza kuwa vikosi vya usalama vya serikali vilizuia mashambulizi ya wanamgambo yaliosababisha vifo vya zaidi ya watu 50.
Mapigano pia yanaripotiwa katika maeneo mengine mengi katika eneo hilo huku wanaharakati na vyombo vya habari wenye kuhusishwa na wanamgambo wakidai kupata udhibiti wa baadhi ya maeneo na kukamata makumi ya wanajeshi.
BBC haijaweza kuthibitisha kwa uhuru madai hayo.
Viunga vya Lalibela, mji mwingine katika mkoa huo ambao ni nyumbani kwa makanisa maarufu, ulishuhudia vurugu wiki iliyopita ambazo zilijumuisha silaha nzito.
Mashambulizi mengi ya ndege zisizo na rubani yameripotiwa katika wiki za hivi karibuni katika maeneo kadhaa.
Kongamano la kila mwaka la ngazi ya juu la amani lililopangwa kufanyika mwezi Oktoba katika mji mkuu wa mkoa huo, Bahir Dar, limetangaza kuahirisha mkutano wake hadi Aprili mwaka ujao likisema ni kutokana na "hali zisizotarajiwa".
Kucheleweshwa kwa mkutano huo, ambao washirika wake ni pamoja na Umoja wa Afrika na UN, kunaweza kuhusishwa na ukosefu wa usalama katika eneo hilo.
Wakati huo huo shirika huru la kutetea haki za binadamu, Baraza la Haki za Kibinadamu la Ethiopia, limeshutumu mamlaka kwa kuendelea kukamata watu kiholela katika mji mkuu, Addis Ababa, ambao ulianza baada ya hali ya hatari kutangazwa mwezi Agosti kukabiliana na ghasia huko Amhara.