Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapadre watatu wauawa katika nyumba ya watawa Afrika Kusini

Mapadre Watatu Wauawa Katika Nyumba Ya Watawa Afrika Kusini Mapadre watatu wauawa katika nyumba ya watawa Afrika Kusini

Wed, 13 Mar 2024 Chanzo: Bbc

Watawa watatu wa Kikoptiki wa Misri "wameuawa kikatili" ndani ya nyumba ya watawa nchini Afrika Kusini, Kanisa limesema.

Padre Takla Moussa, Padre Minah ava Marcus na Padre Youstos ava Marcus waliuawa mapema Jumanne, Dayosisi Kuu ya Afrika Kusini ya Kanisa la Kiorthodoksi la Coptic ilisema katika taarifa.

Muumini wa Kanisa la Misri amekamatwa kama anayeweza kuwa mshukiwa.

Mauaji hayo yameleta mshtuko kote katika jumuiya ya Coptic Orthodox nchini Afrika Kusini na kwingineko.

"Maumivu yetu na huzuni, hakuna kiasi [cha] maneno yanaweza kueleza, lakini tunajua kwamba wanafurahi katika paradiso katika kifua cha Baba zetu Ibrahimu, Isaka na Yakobo," taarifa ya Kanisa ilisema.

Askofu Mkuu Angaelos wa Kanisa la Kiothodoksi la Coptic huko London alielezea mauaji hayo kuwa "ya kuhuzunisha na ya kushtua" .

Waliuawa katika makazi ya watawa Saint Mark and Saint Samuel iliyoko Cullinan, mji mdogo kilomita 30 (maili 18) mashariki mwa mji mkuu, Pretoria.

Wote watatu waligunduliwa wakiwa na majeraha ya kuchomwa visu, msemaji wa polisi wa mkoa Kanali Dimakatso Nevhuhulwi alinukuliwa akisema na shirika la habari la Reuters.

Mtu aliyenusurika aliwaambia polisi kuwa alipigwa na chuma lakini alifanikiwa kutoroka na kujificha.

Polisi bado wanajaribu kubaini chanzo cha mauaji hayo, Kanali Nevhuhulwi alisema, akiongeza kwamba washambuliaji "inaripotiwa kwamba waliondoka eneo la tukio bila kuchukua vitu vyovyote vya thamani".

Viwango vya uhalifu wa kutumia nguvu viko juu nchini Afrika Kusini na nchi hiyo ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani.

Watawa katika Kanisa la Kiorthodoksi la Coptic, mojawapo ya makanisa kongwe zaidi ulimwenguni, hujitolea maisha yao kwa sala na ukuaji wa kiroho.

Chanzo: Bbc