Johannesburg, Afrika Kusini (AFP)
Mtikisa nyavu wa Liverpool, Sadio Mane anatarajiwa kutangazwa kuwa mtu wa kwanza kutingisha habari mwaka 2020 kwa kushinda tuzo ya Mwanasoka wa Mwaka nchini Misri wiki ijayo.
Sherehe zitakazofanyika Januari 7 zitafungua pazi la mwaka unaotarajiw akujaa matukio mengi ndani na nje ya uwanja, kukiwa na michuano ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022 na kuwania tiketi za fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2021.
AFP Sport inaangalia matukio hayo yatakayotawala mchezo huo maarufu katika bara ambalo wanasoka wazuri na viongozi wabovu huchangia jukwaa moja la habari.
Mane, ambaye amekuwa akifunga mfululizo katika klabu yake ya Liverpool na Senegal, anapewa nafasi kubwa ya kuwa mchezaji wa pili katika nchi yake akimfuatia El Hadji Diouf, kutangazwa kuwa Mwanasoka wa Mwaka.
Wapinzani wake, mmoja ambaye wanacheza pamoja klabu ya Liverpool, ni Mohamed Salah, Mmisri ambaye ameshatwaataji hiyo mara mbili zilizopita, na mshambuliaji wa Algeria, Riyad Mahrez wa Manchester City.
Mchezaji wa Mwaka, na washindi wengine wa tuzo saba za wanaume na wanawake, watatangazwa katika sherehe itakayofanyika katika hoteli ya Hurghada.
Kombe la Dunia
Wiki mbili baada ya tuzo hizo, Misri itakuwa mwenyeji wa tukio jingine kubwa, upangaji wa ratiba ya hatua ya makundi ya michuano ya awali ya Kombe la Dunia utakaofanyika jijini Cairo.
Orodha ya ubora inayotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) inategemewa kuamua timu zitakazopewa nafasi, ikimaanisha Senegal, Tunisia, Nigeria, Algeria, Morocco, Ghana, Misri, Cameroon, Mali na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zitakuwa kwenye chungu kimoja.
Mataifa hayo yote, ukiondoa Mali, yameshashiriki fainali za Kombe la Dunia, na Ivory Coast ambayo inaweza kutaka kutumia uwezo mkubwa wa kuchanganya miguu wa Wilfried Zaha, inaweza kuwa ndiyo timu hatari kuliko zote.
Mataifa ya Afrika
Matatizo yalishaanza baada ya kubadili muda wa fainali za Mataifa ya Afrika kutoka Januari/Februari hadi Juni/Julai mwaka huu kuepuka vita baina ya nchi na klabu kuhusu kutumia wachezaji wanaosakata soka barani Ulaya.
Michuano ya kwanza iliyofanyiwa mageuzi ya Klabu Bingwa ya Dunia ikishirikisha klabu 24, imepangwa kufanyika Juni 17 hadi Julai 4, 2021 nchini China, hali ambayo itaharibu fainali za Mataifa ya Afrika ambazo zimepangwa kufanyika katikati ya mwaka nchini Cameroon.
Viongozi waandamizi wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) walisema bila ya kutaka kutajwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kurejesha fainali hizo Januari/Februari, na hilo linaweza kufanya wachezaji wengi kuweka mbele maslahi ya klabu.
Michuano ya Ubingwa wa Mataifa wa Afrika (Chan)
Tunisia imeripotiwa kuwa kutokana na mashindano kuw amengi, imeamua kujiondoa katika fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), ambayo hushirikisha wachezaji wanaosakata soka ndani ya nchi zao, zitakazofanyika mwaka 2020 nchini Cameroon.
Awali michuano hiyo inayofanyika kila baada ya miaka miwili ilipangwa kufanyika Aprili 4 hadi 25 mwaka huu katika majiji matatu tya kusini mwa Cameroon-- mji mkuu wa Yaounde, Douala na Limbe.
Michuano hiyo inayoshirikisha mataifa 16 itatumika kuona kama Cameroon imejiandaa vizuri kwa fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani baada ya kuchelewa kukamilika kwa ujenzi kusababisha fainali za mwaka jana zihamishiwe Misri.
Ligi ya Mabingwa
Mabingwa watetezi, Esperance ya Tunisia wamekuwa katika hali mbaya wakati wakisaka kuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa wa Afrika mara tatu mfululizo, baada ya kuhangaika kuiondoa klabu ya Chad na baadaye kufanya kile isichotarajiwa kwa kuishinda Raja jijini Casablanca.
Imepoteza wachezaji kadhaa nyota waliokuwemo katika kikosi kilichotwaa ubingwa mwaka 2019, akiwemo winga wa Algeria, Youcef Belaili, na kikosi kilichoanza mechi ya makundi mwishoni mwa wiki iliyopita kilikuwa na wachezaji wanne tu Watunisia.
Timu ambayo imeweka rekodi ya kutwaa ubingw ahuo mara nane, Al Ahly ya Misri, TP Mazembe ya Congo DR, Mamelodi Sundowns of South Africa na klabu za Casablanca-- Raja na Wydad-- zinatazamiwa kuwa tishio.
Kombe la Shirikisho
Jina jipya litapatikana mwaka huu kwa kuwa washindi wa hivi karibuni-- Ahly, Etoile Sahel ya Tunisia, Mazembe, Raja na Zamalek ya Misri zote zinashiriki Ligi ya Mabingwa.
Super Cup
Zamalek inatishia kugomea mechi ya Super Cup iliyopangwa kufanyika Februari 14 dhidi ya Esperance na ambayo itachezwa Qatar, nchi ambayo Misri inaituhumu kwa kuyumbisha eneo la Mashariki ya Kati.
Mwenyekiti mtata wa klabu hiyo, Mortada Mansour anasema Zamalek itabadili msimamo wake kama itaagizwa na serikali.
"Sielewi kwa nini CAF inataka mechi ichezwe katika nchi ambayo ni adui wa Misri. Sisi ni klabu za Afrika kw ahiyo kwa nini tuchezee Asia? ," aliuliza Mansour katika mkutano na waandishi wa habari.
CAF
Kipindi cha miezi sita cha katibu mkuu wa Fifa, Fatma Samoura kufanya kazi ofisi za CAF, ambayo ina migogoro, kinaisha Januari 31 na kutakuwa na shauku kubw aya kutaka kujua Msenegali huyo amefanya nini.
Kuwepo kwake CAF kulilenga kuanzisha mageuzi, hasa ya utawala, mashindano, uamuzi na uendeshaji wa jarida la World Soccer.
Aliyekuwa akimsaidia Samoura ni rais wa CAF, Ahmad Ahmad, ambaye hajazungumzia tuhuma zozote zinazoelekezwa kwake, ikiwemo rushwa, matumizi mabaya ya fedha na unyanyasaji wa kingono.
haki za televisheni
Mechi za timu za taifa za nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zimekuwa hazitangazwi moja kwa moja tangu mkataba wa miaka 12 wa televisheni na kampuni ya Ufaransa ulipofutwa.
kampuni hiyo, Lagardere Sports ililipa dola 1 milioni za Kimarekani mwaka 2017 kwa ajili ya haki za masoko na televisheni, lakini uamuzi tofauti ulisema kuwa mkataba huo haukuwa halali kwa sababu hakukuwa na taratibu za zabuni.