Mamlaka ya kitaifa ya udhibiti wa dawa nchini Uganda imekiri kwamba ilijua kwamba dawa za kupunguza makali ya HIV zilikuwa zikitumika kunenepesha Wanyama 2014 lakini halikuonya umma.
Inspekta mkuu wa mamlaka hiyo Amos Atumanya aliambia bunge kwamba walikuwa wanajua kwamba dawa hizo za kukabiliana na virusi vya Ukimwi zilikuwa zikipatiwa nguruwe na kuku ili kuwatibu.
Bwana Atumanya alisema kwamba ilikuwa hatari kwa binadamu kutumia kiwango kidogo cha dawa hizo katika chakula.
Lakini mamlaka hiyo imepuuza matamshi yake.
Msemaji amesema kwamba iwapo kuna hatari yoyote ya kiafya ingeonya umma huku kazi ya mamlaka hiyo ikiwa kudhibiti utumizi wa dawa na sio chakula wala chakula cha Wanyama.
Ripoti ya hivi majuzi kutoka chuo kikuu cha Makerere nchini humo iligundua kwamba zaidi ya thuluthi moja ya kuku na asilimia 50 ya nguruwe waliofanyiwa vipimo walikuwa na chembechembe za dawa hizo za kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi.
Nyama hiyo ilinunuliwa kutoka masoko yaliopo mjini Kampala pamoja na mji wa kaskazini wa Lira.
Akizungumza mbele ya kamati ya bunge kuhusu Ugonjwa wa Ukimwi, bwana Atumanya alisema kwamba mamlaka ya kitaifa ya udhibiti wa dawa NDA ilifanya uchunguzi mwaka 2014 kuhusu matumizi ya dawa za kukabiliana na Ukimwi katika kilimo cha wanyama.
Hata hivyo, licha ya kwamba ripoti ilichapishwa, haikutoa onyo kwa umma kwa hofu ya kuathiri sekta ya uuzaji wa vyakula katika mataifa ya kigeni.
"Hivyo basi tulikuwa tukijaribu kutafuta njia nyingine ya kukabiliana na hali hiyo’’, alisema.
Mhojiwa mmoja wa utafiti huo wa Chuo cha Sayansi ya Afya katika Chuo Kikuu cha Makerere, alisema nguruwe ambao walipewa dawa za kupunguza makali ya VVU "hukua haraka na kunenepa na huuzwa haraka".
Lakini Bw Atumanya alisema jambo hilo linaweza kusababisha matatizo makubwa kwa binadamu waliokula nyama hiyo na kuambukizwa VVU.
"Una uwezekano wa kuwa sugu dhidi ya dawa hizi za ARVs," alisema.
"Katika siku zijazo ikiwa unazihitaji, basi utapata ARV hii haifanyi kazi kwa baadhi."
Takriban watu milioni 1.4 nchini Uganda wanaishi na VVU/UKIMWI, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Ripoti ya NDA mwaka 2014, iligundua kuwa dawa za kupunguza makali ya VVU zilitumika zaidi kutibu homa ya nguruwe Afrika ambayo pia inajulikana kama Ebola ya Nguruwe na kwa sasa haina tiba.
Pia ilithibitisha madai kwamba ARVs zilikuwa zikitumika kutibu ugonjwa wa Newcastle katika kuku.
Kufuatia matamshi ya Bw Atumanya, hata hivyo, msemaji wa NDA alitetea uamuzi wake wa kutotangaza matokeo yake.
"NDA ina jukumu la kudhibiti dawa, sio chakula au chakula cha mifugo," alisema.
"Ikiwa kulikuwa na tishio lolote la afya ya umma kuhusu dawa zinazotumiwa, NDA itakuwa ya kwanza kutoka na kuonya umma kama tunavyofanya siku zote.
"NDA inasalia kuwa macho na imejitolea kuhakikisha kwamba Waganda wanapata dawa salama, zinazofaa na zenye ubora."
Aliongeza kuwa mdhibiti huyo alianzisha hatua kadhaa za kukomesha utumizi mbaya wa dawa za kulevya, jambo ambalo lilisababisha watu kadhaa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.