Juni 20, kila mwaka dunia inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilizindua siku hii mwaka 2000, na tangu wakati huo, jumuiya ya kimataifa imetumia siku hiyo kuangazia njia za kuboresha maisha ya wakimbizi.
Nchi Kenya, kambi ya wakimbizi ya Dadaab sasa ni makazi ya zaidi ya wakimbizi 320,000 na wanaotafuta hifadhi.
Wengine zaidi wakiwasili kila siku kutoka nchi jirani ya Somalia. Idadi yao imeongezeka kwa kasi katika miezi ya hivi karibuni kutokana na ukame wa muda mrefu nchini Somalia, na kusababisha msongamano mkubwa wa watu na kuongezeka kwa shinikizo kwa huduma zilizopo, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa maji ya kunywa na vyoo.
Serikali ya Kenya pamoja na UNHCR, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, na mashirika mengine ya misaada ya kibinadamu wanawasaidia wakimbizi wapya wanaowasili kwa kuwapatia huduma za msingi ikiwa ni pamoja na chakula, maji na huduma za afya.
Serikali ya Kenya ililazimika tena kufungua kambi ya nne, Ifo 2, ili kuwahudumia wakimbizi wapya wanaowasili na kupunguza matatizo ya rasilimali katika kambi zilizopo.
Mwaka 2019 Kenya iliifunga kambi ya IFO 2 na Kambioos baada ya wakimbizi kujitolea kwa hiari yao kurejea nchini Somalia. Lakini mgororo wa kivita na hali ya ukame imewalazimu wakimbizi kukimbilia Kenya ili kutafuta chakula na makazi.
Kila kukicha Wakimbizi wanalazimika kuacha nyumba zao kwa sababu ya vita, ugaidi, au majanga mengine—lakini kukimbia nchi yao mara nyingi ni mwanzo tu wa safari ngumu.
Wakimbizi wengi hujikuta wakiishi katika kambi hadi wapate makazi mapya—baadhi yao wakipitia hali ngumu kwa kukosa vifaa vya kutosha kwa ajili ya kuishi kwa muda mrefu.
Wakimbizi wanaotafuta hifadhi katika mataifa mengine mara nyingi hawana usemi katika nchi ambayo hatimaye wamehamishwa, na mchakato wa ukiritimba unaohusika katika kutafuta makazi yao mapya unaweza kuchukua miaka.
Kila mwaka ifikapo tarehe 20 Juni, ulimwengu huadhimisha siku ya wakimbizi kuonyesha nguvu na ujasiri wa watu ambao wamelazimika kukimbia nchi yao ili kuepuka migogoro au mateso.
Kauli mbiu ya 2023 ya Siku ya Wakimbizi Duniani ni "matumaini mbali na nyumbani."