Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema mamia ya watu wameuawa katika mapigano ya kikabila katika eneo la Darfur Magharibi nchini Sudan.
Volker Turk amesema, "Mashambulizi yaliyochochewa kikabila huko Darfur Magharibi na yaliyofanywa na Vikosi vya Radiamali ya Haraka vya Sudan RSF pamoja na wanamgambo waitifaki wao wa Kiarabu, yamepelekea kuuawa mamia ya Wasudan wasio Waarabu hasa wa jamii ya Masalit."
Afisa huyo wa UN amesema mauaji hayo yanakumbusha mauaji ya watu zaidi ya laki tatu katika mgogoro wa Darfur baina ya mwaka 2003 na 2008, huku akisisitiza kwamba, umwagaji damu wa aina hiyo haupasi kujikariri.
Amesema mashambulizi hayo mapya yameripotiwa zaidi katika mji wa El Geneina, makao makuu ya jimbo la Darfur Magharibi, ambao sehemu yake kubwa inadhibitiwa na wapiganaji wa RSF. Mashambulizi Darfur
Mapigano ya kuwania madaraka nchini Sudan yalianza Aprili 15 kati ya vikosi vya Jeshi na vya Usaidizi wa Haraka RSF; na juhudi za upatanishi wa kimataifa za kumaliza vita na mapigano hayo na kuzileta pande zinazozozana kwenye meza ya mazungumzo hadi sasa hazijazaa matunda.
Haya yanajiri siku chache baada ya watu zaidi ya 40 kuuawa katika mashambulizi ya anga yaliyoripotiwa kufanywa na jeshi la Sudan huko kusini mwa Khartoum, mji mkuu wa hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.