Mamia ya watu walishiriki katika mazishi ya mwandishi wa habari John William aliyefariki katika ajali ya gari, huku mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yakitaka uchunguzi huru kuhusu kifo chake.
Wanahabari wengi nchini humo, marafiki, na wanafamilia walishiriki katika mazishi haya siku ya Jumapili, huku kukiwa hakuna mengi yaliyosemwa kuhusu kazi ya marehemu au jinsi kifo chake kilivyotokea.
Frank Habineza kutoka chama cha upinzani cha Democratic Green Party of Rwanda, Victoire Ingabire na Bernard Ntaganda ni miongoni mwa wanasiasa waliohudhuria mazishi hayo.
"Hatutasahau mchango wako wa thamani katika kukuza uhuru wa vyombo vya habari katika mazingira yenye changamoto", Bi Ingabire alisema kuhusu kifo cha Bw Ntwali.
Polisi walisema Bw Ntwali alifariki papo hapo kwenye ajali ya barabarani siku ya Jumanne usiku wakati bodaboda aliyokuwa amepanda ilipogongwa na gari, dereva akakamatwa, polisi waliongeza.
Lakini Human Rights Watch ilisema kwamba "kuna sababu nyingi za kutilia shaka" maelezo ya polisi na kutaka "utaalamu wa kimataifa kubaini kama aliuawa au la."
Mwandishi huyu ni nani?
rwanda BBCCopyright: BBC Bwana Ntwali, aliyekuwa na miaka 43, baba wa mtoto mmoja alizaliwa kusini mwa Rwanda na kukulia mji mkuu wa Kigali ambako alianza kazi yake ya uandishi wa habari baada ya kumaliza masomo yake ya chuo kikuu.
Alifanya kazi katika radio mbalimbali za nchini humo, magazeti na katika mitandao ya habari, kifo kilipomkuta alikuwa mhariri wa The Chronicles, lakini pia alimiliki chaneli ya YouTube inayoitwa Pax TV – Ireme News.
Bwana Ntwali alikuwa mkosoaji mkubwa wa mamlaka yaliyopo madarakani na chama tawala katika ripoti zake akiangazia haki hali ambayo ilifanya apate vitisho na unyanyasaji, alisema.
Alikuwa na uwezo wa kuhoji waziwazi sera za serikali kama vile kuhamishwa kwa watu kwa ajili ya mradi unaomilikiwa na watu binafsi, kodi ya ardhi, kukamatwa kwa wanachama wa upinzani na wamiliki wa chaneli za YouTube, au kifo cha mwimbaji Kizito Mihigo.
Wakosoaji wake wangemwita "mwandishi wa habari mwenye msimamo mkali".
Bw Ntwali hapo aliwahi kunusurika na "ajali za barabarani" na "vitisho vya kifo kutoka kwa maajenti wa serikali", na mamlaka haikuzungumzia madai yake. "
"Anaingia kwenye orodha ndefu ya watu ambao wameipinga serikali na kufariki katika mazingira ya kutiliwa shaka," Lewis Mudge mkurugenzi wa Afrika ya Kati katika Human Rights Watch alisema juu ya kifo chake.
"Ntwali alituambia kuhusu ajali za barabarani ambazo zilijaribiwa katika maisha yake, inatisha jinsi sasa tunamzika baada ya ajali ya barabarani," mwandishi wa habari aliyeenda kumzika aliiambia BBC.