Mamia ya wakazi wa mji wa Derna mashariki mwa Libya waliandamana Jumatatu dhidi ya viongozi wa eneo hilo, zaidi ya wiki moja baada ya mafuriko makubwa kuua maelfu ya watu katika mji huo.
Waandamanaji hao walimkosoa kiongozi wa bunge la mashariki mwa Libya, Aguila Saleh, na mamlaka za mitaa ambazo walilaumu kwa mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya karibu watu 4,000, kulingana na takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa ya pamoja, waandamanaji hao walisema wanataka uchunguzi wa haraka kuhusu maafa hayo na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya viongozi waliohusika.
Pia walidai fidia, uchunguzi juu ya fedha za jiji na ujenzi wa Derna.
Mashariki mwa Libya inatawaliwa na serikali nyingine, tofauti na serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa yenye makao yake makuu katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Wataalamu kadhaa na mashirika ya kibinadamu yamependekeza kuwa mafuriko yangeweza kuzuiwa ikiwa mamlaka za mitaa ziliwahamisha wakazi au angalau kutoa onyo kuhusu kimbunga Daniel.
Wataalamu pia wamesema kuwa kutelekezwa kwa mabwawa ya jiji hilo na mamlaka kulisababisha kubomokwa kwa mabwa hayo yaliyosababisha mafuriko yalipoporomoka.
Waandamanaji pia walichoma nyumba ya meya wa Derna, Abdulmenam al-Ghaithi. Bw Ghaithi, pamoja na maafisa wengine wa manispaa ya Derna, wamesimamishwa kazi na Waziri Mkuu wa mashariki mwa Libya Osama Hammad.