Sakata la uhasama kati ya Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Serikali ya Rais William Ruto limeendelea kuchukua sura tofauti, baada ya Kenyatta kudai kwamba maofisa wa Serikali walitaka kuweka silaha na dawa za kulevya kwenye nyumba ya mwanaye ili wamkamate kama mhalifu.
Kenyatta alitoa tuhuma hizo juzi, zikiwa zimepita siku chache baada ya polisi kuvamia nyumbani kwa mwanaye, Jomo Kenyatta, wakiwa kwenye gari lenye namba za usajili za Sudan Kusini.
Tukio hilo lililotokea Ijumaa iliyopita, lilimuibua Kenyatta hadharani akimtaka Rais Ruto na Serikali yake waache kuifuatilia familia yake. Ameweka bayana kama wanamtaka yeye basi waende kwake moja kwa moja badala ya kuisumbua familia yake.
Kabla ya tukio hilo, mjane wa mwasisi wa Taifa hilo, Mama Ngina Kenyatta ambaye ni mama yake mzazi na Uhuru Kenyatta aliondolewa walinzi wake wote ambao amekuwa nao kwa muda mrefu, jambo ambalo limemuudhi Rais huyo mstaafu anayemuunga mkono kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.
Sakala hilo limefika hapo baada ya mfululizo wa maandamano ya wananchi yanayofanyika nchini humo yakiongozwa na Raila, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kupinga kupanda kwa gharama za maisha na kuibiwa kwa uchaguzi.
Rais Ruto anamtuhumu Kenyatta kufadhili maandamano hayo yaliyosababisha vifo vya watu 12 hadi sasa na uharibifu wa mali, madai ambayo yeye ameyakanusha akisema Serikali ishughulikie madai ya wananchi badala ya kumwandama yeye na familia yake.
Jumatatu iliyopita, Kenyatta alikutana na wahariri wa vyombo vya habari na kuzungumzia madai ya Serikali ya kuhifadhi bunduki, zinazodaiwa kushikiliwa na watoto wake wawili; Jomo na Muhoho. Alikanusha madai hayo, akisema watoto wake wanamiliki silaha sita kihalali.
Baada ya askari kwenda kwenye nyumba ya Jomo, Serikali ilithibitisha kuvamia nyumba tatu katika eneo la Karen jijini Nairobi kutafuta bunduki 23 zinazodaiwa kutumika kutekeleza operesheni haramu nchini wakati wa maandamano ya kuipinga Serikali.
Hata hivyo, licha ya familia yake kutuhumiwa kumiliki silaha hizo 23, Kenyatta alisema kulikuwa na mpango wa kumwekea bunduki na dawa za kulevya wakati wa operesheni ya Ijumaa iliyopita.
“Suala hili la bunduki limejaa propaganda nyingi ili kugeuza mawazo kutoka kwa kile ambacho kimekuwa kikitokea nchini.
“Ninaamini walitaka kuweka dawa na bunduki katika nyumba ya mwanangu,” Kenyatta aliwaambia waandishi wa habari.
Kenyatta, aliyejawa na hasira anasema tukio hilo lilimuumiza. Alisema: “Nilienda kwa sababu nilipigiwa simu na mwanangu. Sikuwa mlevi, niliumia sana.”
Rais huyo wa zamani alidai kuwa wanawe wawili wanamiliki bunduki sita kwa jumla, tatu kila mmoja na kwamba bunduki zote zimesajiliwa kisheria. Alifafanua kuwa binti yake, Ngina, yeye hamiliki bunduki.
Kwa mujibu wa Rais huyo wa zamani, hakuna hata mmoja wa wanawe ambaye amepokea amri ya kusalimisha silaha zake kama inavyodaiwa kwenye vyombo vya habari na maofisa wakuu wa Serikali.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki alisema vyombo vya usalama vimepewa jukumu la kupekua eneo hilo kama sehemu ya operesheni pana inayolenga kuwaondoa watu walio na silaha na viongozi wa magenge ya uhalifu yanayojulikana.
Kenyatta pia alibainisha kuwa amelazimika kutumia walinzi binafsi nyumbani kwa mama yake baada ya walinzi wa Mama Ngina kuondolewa na Serikali.
“Stahiki ambazo mama yangu anapata si kwa sababu yangu, bali ni kwa sababu yeye ni mke wa Rais wa zamani,” alisema.
“Tumelazimika kuajiri walinzi binafsi,” alisema Rais huyo wa zamani.
Maandamano yasitishwa
Wakati huohuo, Muungano wa Azimio la Umoja umesitisha maandamano ya kuipinga Serikali yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchini kote leo.
Katika taarifa iliyotolewa juzi, muungano huo ulisema badala ya kuingia mitaani, watafanya gwaride la mshikamano na mkesha kwa waathirika wa ukatili wa polisi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Muungano huo umewahimiza wafuasi wake kujitokeza na kuwasha mishumaa na kuwawekea maua waathirika wa ukatili wa polisi wakati wa hafla hiyo.
Azimio hilo limeleeza kwenye taarifa yake kwamba hadi sasa vifo 50 vimeripotiwa, huku mamia ya watu wakijeruhiwa na wamelazwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya.
Hata hivyo, idadi rasmi ya waliouawa kwenye maandamano hayo bado haijatolewa na Serikali.
“Azimio tumefanya uamuzi kwamba Jumatano, badala ya kwenda mitaani kwa maandamano ya amani kama tulivyotangaza hapo awali, tutafanya maandamano ya mshikamano na mkesha kwa waathirika wa ukatili wa polisi katika maeneo mbalimbali katika maeneo yote ya nchi,” ilisema taarifa hiyo.
“Tunawahimiza Wakenya wajitokeze kuwasha mishumaa na kuweka maua kama ishara ya kuwakumbuka na kuwaheshimu waathirika...tunawahimiza Wakenya kusali na kusoma majina ya waathirika wa ukatili huo. Tutatoa orodha yao kwa wakati kwa ajili ya shughuli hiyo,” inaeleza taarifa hiyo ya Azimio la Umoja.
Polisi kushtakiwa
Tume ya Kutathmini Utendaji Kazi wa Polisi nchini Kenya (IPOA) imesema imewasilisha mafaili kadhaa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kuwafungulia mashtaka maofisa wa polisi kwa kuvunja sheria wakati wa kukabiliana na waandamanaji nchini Kenya.
Kwa wiki kadhaa sasa, Kenya imeshuhudia maandamano yanayoongozwa na upinzani nchini kupinga kupanda kwa gharama za maisha, na polisi wamelaumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi katika kukabiliana na hali hiyo.
Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu (Amnesty International) liliripoti vifo vya watu zaidi ya 30, tangu kuanza kwa maandamano hayo.
Kamishna wa IPOA, Joshua Waiganjo aliliambia Shirika la Utangazaji la BBC kwamba ofisi yao imekuwa ikituma maofisa kwa siri ili kujionea utendaji kazi wa polisi.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki alisisitiza kwamba polisi wataendelea kutumia kila mbinu inayofaa kukabiliana na wanaopora mali za watu na kutekeleza uhalifu.
Alionya kwamba kuna wahalifu wanaohujumu usalama na uchumi wa nchi na wanatumia maandamano kutekeleza uovu wao.