Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo yaiva ujenzi bomba la mafuta Tanzania, Uganda

0f78534a4d07e48b184d9f83990d8c8c.jpeg Mambo yaiva ujenzi bomba la mafuta Tanzania, Uganda

Tue, 2 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UJENZI wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (Eacop) kutoka Hoima, Uganda mpaka Tanga, Tanzania kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 3.5 utaanza mwezi huu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Palamaganda Kabudi alisema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu ziara yake rasmi ya siku tano nchini Ufaransa.

Alisema Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafuta ya Total Oil Afrika, Nicolas Terraz alimhakikishia kuwa ujenzi rasmi wa mradi huo utaanza wiki ya pili ya Machi.

"Nilipokuwa Ufaransa nilifanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Total ambaye alinihakikishia kuwa mipango iko tayari kwa ajili ya ujenzi wa bomba kuanza wiki ya pili ya mwezi ujao," alisema.

Septemba mwaka jana Rais John Magufuli na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni walikubaliana kuharakisha utekelezaji wa mradi wa Eacop katika mazungumzo yao yaliyofanyika Chato mkoani Geita.

Mazungumzo hayo yalifanyika baada ya Uganda kutia saini Mkataba wa Serikali Mwenyeji (HGA) kwenye Mradi wa Eacop.

Viongozi hao wawili waliwahimiza maofisa kutoka nchi zote mbili, kuharakisha kukamilisha masuala mbalimbali ambayo hayajakamilika ikiwemo HGA ya Tanzania ili kuanza utekelezaji wa mradi huo.

Oktoba mwaka jana Tanzania na Total walitia saini makubaliano, ambayo yanaweza kufungua njia ya ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,447 litatumika kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga ili kusafirishwa nje ya nchi.

Kabudi alisema theluthi mbili ya bomba hilo itapita Tanzania. Alisema mradi huo utazalisha angalau ajira 4,700 za moja kwa moja na nyingine 7,000 zisizo za moja kwa moja.

Tanzania na Uganda zilikubaliana Machi 2016 kuwa bomba la kusafirisha mafuta yasiyosafishwa kutoka Bonde la Ziwa Albert Magharibi mwa Uganda hadi kwenye masoko ya ng'ambo yapitishwe kupitia Bandari ya Tanga.

Mkataba huo ulisainiwa na nchi hizo mbili jirani Mei, 2017 na kufuatiwa na uwekaji wa jiwe la msingi katika Bandari ya Tanga na marais Magufuli na Museveni Agosti mwaka huo huo.

Chanzo: habarileo.co.tz