Mambo yanazidi kuwa magumu kwa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa anayeandamwa kwa tuhuma za ufisadi na utakatishaji fedha.
Katikati ya sakata hilo, amemsimamisha kazi mkuu wa ofisi ya kukabiliana na ufisadi baada ya mkuu huyo kuanzisha uchunguzi wa tuhuma za utakatishaji fedha dhidi yake.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Afrika Kusini mwishoni mwa wiki ilisema “Wakili Busisiwe Mkhwebane ataendelea kusimamishwa kazi hadi mchakato ulioanza bungeni utakapokamilika na nafasi yake inashikiliwa na naibu wake.”
Hata hivyo, Ofisi ya Rais iliongeza kuwa kutokuwepo kwa Mkhwebane ofisini hakutazuia uchunguzi wowote ambao aliuanzisha dhidi ya Rais Ramaphosa.
Taarifa hiyo ya Ikulu ilitolewa siku moja tangu Mkhwebane aanzishe uchunguzi dhidi ya Ramaphosa kuhusu tuhuma za kuficha tukio la wizi wa fedha uliofanyika kwenye nyumba iliyopo shambani kwake mwaka 2020.
Mahasimu wa Ramasphosa wanasema kashfa hiyo iliibua mpango wa kutakatisha fedha unaofanywa na Rais huyo, kwa kuwa wezi walioingia kwenye nyumba yake walikuta fedha taslimu Dola 4 milioni za Marekani zikiwa zimefichwa kwenye samani za nyumba hiyo.
Bunge linalotawaliwa na chama cha Ramaphosa (ANC) lilianzisha mchakato wa kumwondoa kwenye nafasi yake mkuu huyo wa kupambana na ufisadi, ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo na mtangulizi wa Ramaphosa, Jacob Zuma.
Kuteuliwa kwa Mkhwebane kulitazamwa na wengi kama jaribio la kumlinda Zuma dhidi ya madai ya ufisadi. Kwa miaka kadhaa amekuwa akifungua kesi na kushindwa akijaribu kuzuia kuondoshwa kwenye nafasi yake.
Wakati Ramaphosa akitangaza kumsimamisha kazi Mkhwebane, kambi ya upinzani ilichachamaa bungeni juzi ikimtaka Rais huyo ajiuzulu kupisha uchunguzi wa uhalifu dhidi yake kwa kuficha wizi uliofanyika nyumbani kwake.
Wabunge wa Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) waliondolewa kwa nguvu bungeni kwa kuingilia kila mara hotuba ya Rais Ramaphosa alipokuwa akiwasilisha bajeti ya ofisi yake.
Mmoja wa wabunge hao, Natasha Ntlangwini alisema kwa nguvu bungeni: “Hatuwezi kuhutubiwa na mtakatishaji fedha na mhalifu. Hatuwezi kuhutubiwa na mtu anayetuhumiwa kutenda makosa makubwa ya uhalifu.”
Wizi huo wa mwaka 2020 uliofanyika kwenye nyumba yake iliyo katika jimbo la kaskazini la Limpopo, kwa mara ya kwanza uliandikishwa mwezi huu na mkuu wa zamani wa ujasusi, Arthur Fraser.
Baadaye, Ramaphosa alithibitisha juu ya wizi huo akisema fedha hizo dola 4 milioni taslimu zilikuwa malipo aliyopata kwa kuuza wanyama kwenye kitalu chake.
Alidai kuwa aliripoti kwa mkuu wa kikosi chake cha ulinzi lakini si kwa polisi.
Apambana na watu wake
Rais Ramaphosa alitazamwa kama mkombozi wa ANC alipoingia madarakani mwaka 2018. Hata hivyo, imani ya tabaka la wafanyakazi na maskini, kwake inazidi kushuka.
Kwa mfano, ni wafanyakazi wachache waliojitokeza kumsikiliza Ramaphosa katika mkutano wa Mei mosi katika Jimbo la Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini. Wale waliohudhuria walimshambulia kwa nyimbo wakisema “Cyril lazima aondoke!”
Makabiliano hayo na Rais katika uwanja wa Royal Bafokeng, yalihusisha wafanyakazi wengi waliofanya mgomo katika mgodi wa dhahabu wa Sibanye-Stillwater ulio karibu na Rustenburg pamoja na wale wanaounga mkono madai ya wachimba madini ya kutaka malipo bora zaidi.
Kitendo cha Ramaphosa kurudi haraka katika lori la polisi lililokuwa na silaha kilionyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni.
Kwa haraka, Rais huyo alitoa taarifa akielezea haja ya kuwepo suluhu ya haki ya mishahara kwa wachimbaji hao.
Hata hivyo, wafanyakazi wengi walikataa kuamini ahadi hizo na kusema wanaunga mkono hatua za umati za kumpinga Rais Ramaphosa katika hafla za Mei mosi.
Vyama vya siasa na wachambuzi wanafuatilia kwa makini hali hiyo. Si tu katika uchaguzi mdogo wa manispaa unaoendelea kwa sasa katika majimbo matatu, bali vita vya ndani vya mamlaka vinapamba moto ndani ya ANC na Ramaphosa anakabiliwa na jitihada za kuchaguliwa tena kama kiongozi wa chama hicho mwaka ujao.
Brian Sokotu, mchambuzi wa siasa mwenye makazi yake Johannesburg, alieleza kuwa Rais Ramaphosa anapoteza imani miongoni mwa wafanyakazi ambao wanataka masuala nyeti yashughulikiwe na Serikali.
Wakati wa enzi za ubaguzi wa rangi, Rais Ramaphosa alikuwa kiongozi wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi wa Migodini (NUM). Alijulikana kwa kupenda maisha ya kifahari, kufurahia mvinyo na tabia yake ya kupanda ndege daraja la kwanza.