Mamake mtoto wa miaka mitatu aliyeshambuliwa Kisii amekamatwa na makachero kwa madai ya kutelekeza majukumu yake ya ulezi.
Mtoto huyo alitekwa nyara na genge la majambazi ambao walimtoa macho yake na kisha kutupa mwili kwenye shamba la migomba ya ndizi.
Mtoto huyo alitoweka Jumatano Disemba 14 kabla ya kupatikana kwenye shamba hilo huku akivuja damu kutokana na kutolewa macho na washambulizi hao.
Mamake mtoto huyo, Maureen Nyaboke, alionekana mara ya kwanza Jumapili Disemba 18 tangu kisa hicho cha mwanawe Sagini.
Alikuwa amefika katika hospitali ya Kisii Eye Care ambapo Sagini anapokea matibabu madaktari wakijaribu kusaidia hali.
Madaktari wanasema mtoto huyo sasa atasalia bila uwezo wa kuona katika maisha yake yote kutokana na shambulizi hilo.
Polisi walimkamata Nyaboke na kumpeleka katika kituo cha polisi cha Nyanchwa ambapo kisa chake kimerekodiwa nambari 33/18/12.
Kwa sasa makachero wamesema anazuiliwa katika kituo cha Rioma akisubiri kustakiwa kwa kutelekeza majuku yake.