Mwanamke mwenye umri wa miaka 58 alifariki dunia akisubiri huduma za matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Nanyuki mnamo Jumatatu, Mei 31.
Halima Hassan alikimbizwa katika hospitali hiyo na jamaa zake baada ya kuanza kuugua akiwa nyumbani.
Alipomwona daktari katika kitengo cha dharura cha hospitali hiyo, aliagizwa kufanyiwa vipimo vya maabara ambavyo alipelekwa na mtoto wake Ramadhan Hassan Omar.
"Mara kadhaa, nilimwendea muuguzi wa kiume kuomba msaada ambaye alihisi nilikuwa nikisumbua na akanijibu kwa ujeuri, ” Omar aliiambia K24 Digital.
Aliongeza kuwa sio yeye peke yake aliyekuwa kwenye foleni kwani kulikuwa na wagonjwa wengine ambao walikuwa wakisubiri matokeo yao.
Omar aligundua baadaye kuwa wahudumu wa maabara na wauguzi walikuwa wakihudhuria sherehe ya kuzaliwa ya mmoja wao katika mojawapo ya vyumba katika hospitalini hiyo.
Afisa wa Afya kaunti ya Laikipia Rose Maitai alithibitisha kisa hicho na kusema kuwa wahusika watachukuliwa hatua kali.
Katika kituo hicho hicho, mama wa watoto wawili alisemekana kuaga dunia baada ya kuvuja kwa muda mrefu.
Kulingana na familia yake, mama huyo mwenye umri wa miaka 24 hakupokea huduma kwa wakati wote aliokuwa akisubiri hospitalini humo.
Wanadai kwamba alihitaji kuongezewa damu ambayo licha ya wasamaria wema 7 kutoa damu, hospitali hiyo iliktaa kumhumia kwa sababu ilikuwa holidei ya kitaifa.
Familia hiyo sasa inadai kwamba hospitali hiyo ilikataa kumsaidia mama huyo ambaye amewaacha watoto wawili wenye umri wa wiki 3 na mwaka 1 mtawalia.
Visa vya utepetevu dhidi ya wagonjwa vimekuwa vikigonga vichwa vya habari kwa muda mrefu sasa.
Itakumbukwa kwamba mwaka wa 2020 mgonjwa alipoteza maisha yake eneo la kuegesha magari katika hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) baada ya kukosa kuhudumiwa kwa saa kadhaa.
Siku moja baadaye, mwanamke mmoja aliyekuwa na majonzi alinaswa kwenye kamera akiwasihi wahudumu wa KNH kumhudumia mgonjwa aliyekuwa katika hali mbaya.
Alihofia kwamba mgonjwa aliyemleta kwa matibabu angeaga dunia ikiwa hataangaliwa haraka.
Hata hivyo wahudumu wa afya hawakuweza kumhudumia mgonjwa huyo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsaApp: 0732482690.