Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama aliyejifungua mapacha atakiwa kuua wanaye ili kutuliza mizimu ya mababu

Eliza Mapacha Elizabeth Cikutsu na wanaye

Tue, 26 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanamke mmoja kutoka kijiji cha Shingoto, eneo bunge la Shinyalu Kaunti ya Kakamega anaishi na uwoga baada ya mumewe kutishia kumfukuza nyumbani kwao kwa sababu kujifungua mapacha.

Mwanamke huyo anakabiliwa na matatizo hayo kwa sababu, kulingana na jamii ya Isukha, ni mwiko kwa mwanamke kuzaa mapacha kama kifungua mimba. Kuzaliwa kwao kunachukuliwa kuwa ishara ya laana (tsishiri) kutoka kwa mababu.

Masaibu ya Elizabeth Cikutsu, 33, yalianza miaka saba iliyopita baada ya kukataa mwito wa kumuua mmoja wa watoto wake mapacha ili kutuliza mila za jamii yao.

“Mama mkwe alikataa kuwanyoa na kuwapa majina walipofikia umri unaotakiwa, nililazimika kuwanyoa mwenyewe kuwapa majina. Mukhwana na Mulongo ni majina ambayo iliashiria ni mapacha,” alisema Cikutsu.

Kukataa kwake kumuua mmoja wa watoto hao kulimfanya akabiliane na matatizo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuchapwa viboko huku mmoja wa mapacha wake akitekwa nyara na na kutaka kuuawa.

“Wakiwa na miezi mitatu nikiwa naoga nilisikia mtoto akilia kwa uchungu, kutokana na shauku ya kutaka kujua nilishtuka kumuona bibi yao akimnyonga mdogo wake, nikawaita majirani waliokuja kunisaidia.

"Mbali na hilo, hivi majuzi alimteka nyara mmoja wa mapacha hao na kumfungia nyumbani kwake kwa siku tatu. Niliripoti kesi kwa chifu, ambaye alinisaidia kumrudisha mwanangu. Suala hilo, hata hivyo, lilitatuliwa katika ngazi ya kifamilia," aliongeza.

Elizabeth aliolewa na Cyrus Cikutsu, 37, na licha ya wanandoa hao kuwa wamejaliwa mapacha, pia ni wazazi wa watoto wengine wawili.

“Mume wangu anakubaliana na mama'ke, amenishutumu mara kadhaa kwa kuwa mjinga akitishia kuoa mwanamke mwingine iwapo nitakosa kufuata mila ya Isukhas, hanisaidii kwa lolote kulea watoto wangu,” aliongeza mama huyo.

Elizabeth anategemea pesa kutokana na kazi ya kijungu jiko anayofanya kwa majirani zake, ikiwa ni pamoja na kulima, kupalilia na kuchota maji ili kukidhi mahitaji yao na ya watoto wake. Jitihada zake za kurejea kwa wazazi wake zimeambulia patupu kwani ni yatima na wazazi walipofariki ndugu zake waliuza shamba na kuhamia kwingine.

Kulingana na mila za Isukha, mara tu mama anapojifungua mapacha, mdogo anatakiwa kuuawa au kutengwa na jamii ili kuepusha baba wa watoto hao kufariki wakiwa na umri mdogo.

"Mdogo anapaswa kuuawa kabla hajatimiza miaka minane la sivyo baba yao ataugua ghafla na kufa, wanachukuliwa kuwa watoto haramu," alisema James Amunze, mzee wa jamii hiyo.

Tambiko fulani hufanywa na wazee wa jamii kwa pacha huyo ambaye baadaye atauawa kabla ya baadhi ya matambiko kufanywa juu ya mwili huo uliozikwa kwenye kichuguu.

Wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 80 wanatupa kuku wawili juu ya paa la nyumba iliyoezekwa kwa nyasi, kila kuku akiashiria mmoja wa mapacha hao, kuku wa mwisho akishuka kwenye paa kuashiria kwamba pacha aliyezaliwa mwisho atauawa.

Ujio wa mambo ya utandawazi yameondoa mila hii ambayo sasa inaitwa jinai na imepitwa na wakati.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live