Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mali yatangaza fungu kusaidia masikini, kampuni kuikabili corona

Mali yatangaza fungu kusaidia masikini, kampuni kuikabili corona

Sat, 11 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita ametangaza kutenga fungu la fedha za kusaidia wananchi masikini na kampuni zilizoathiriwa na ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19, huku maambukizi yakizidi kuongezeka katika taifa hilo la Afrika Masharibi linalosumbuliwa na vita.

Rais alionya Ijumaa kwamba uchumi wa nchi hiyo, ambao tayari umeharibiwa na vita, unakabiliwa na mshtuko na kutangaza fungu la dola 832 milioni kwa ajili ya kuunusuru.

"Serikali ya Mali... imepania kujitoa muhanga kupunguza athari za ugonjwa huu katika uchumi wetu na jamii," Keita alisema katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni. Mali ni moja ya nchi masikini zaidi duniani na imekuwa ikipambana na mashambulizi ya vikundi vya kigaidi ambavyo vimeshaua maelfu ya raia na wanajeshi.

Vita hiyo, ambayo imeacha sehemu kadhaa za nchi kutodhibitiwa na serikali -- imezidisha hofu katika kipindi ambacho Mali inataka kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona.

Mamlaka zimetangaza maambukizi 87 hadi sasa huku kukiwa na vifo saba. Serikali ilishatangaza amri ya kuzuia watu kutembea usiku na ikafunga mipaka ya ardhini.

Akionya kuongezeka kwa kasi kwa gharama zinazohusiana na ugonjwa huo, Keita alisema Ijumaa kuwa serikali itabeba mzigo wa malipo ya maji na umeme kwa familia masikini katika mwezi Aprili na Mei, ikiwa ni kati ya mipango hiyo ya kusaidia wananchi.

Pia Soma

Advertisement
Serikali pia itasambaza tani 56,000 za nafaka kama msaada wa chakula na tani 16,000 za chakula cha mifugo, na kuruhusu marejesho ya kodi kwa kampuni zilizoathiriwa vibaya na virusi hivyo.

Licha ya kuonyesha umuhimu wa wananchi kutokaribiana, Keita alisema raundi ya pili ya uchaguzi wa wabunge itafanyika Aprili 19 kama ilivyopangwa.

Rais huyo pia alisema serikali yake inafikiria kuutenga mji mkuu wa Bamako, ambako maambukizi mengi yamegundulika, akisema uamuzi unatarajiwa mapema.

Chanzo: mwananchi.co.tz