Utawala wa kijeshi nchini Mali umepiga marufuku mashirika yote yasiyo ya kiserikali ambayo yanafadhiliwa au kuungwa mkono na Ufaransa kufanya kazi nchini humo.
Makundi ya misaada ya kibinadamu yamejumuishwa katika marufuku hiyo.
Katika taarifa yake, mamlaka hiyo ilisema hatua hiyo ilifuatia uamuzi wa Ufaransa kusitisha msaada wa maendeleo kutokana na madai ya Bamako kutumia wanajeshi wa kundi la Wagner la Urusi.
Waziri Mkuu wa mpito wa Mali, Kanali Abdoulaye Maïga, alikanusha madai hayo, akisema yanalenga kuivuruga nchi.
Alisema Warusi walikuwa wakifanya kazi kama wakufunzi.
Miezi mitatu iliyopita Paris iliwaondoa wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa wakishirikiana na Mali kukabiliana na makundi ya wanajihadi.