Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mali yafuta Kifaransa kama lugha rasmi nchini humo

FRANCEE ET ALLIES Mali yafuta Kifaransa kama lugha rasmi nchini humo

Tue, 25 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Mali imeamua kukifuta Kifaransa kuwa lugha rasmi nchini humo, na sasa kitatambulika tu kama lugha ya kufanyia kazi.

Mali imechukua uamuzi huo wa kukishusha hadhi Kifaransa kwa mujibu wa Katiba mpya iliyopasishwa katika kura ya maoni ya Juni 18 mwaka huu, ambapo asilimia 96.91 ya Wamali walioshiriki kwenye zoezi hilo walipiga kura ya kuiunga mkono.

Bamako imeamua kukifuta Kifaransa kama lugha rasmi na kukishusha hadhi na kuwa lugha tu ya kufanyika kazi, wakati huu ambapo mivutano katika uhusiano baina ya baraza tawala la kijeshi la Mali na serikali ya Ufaransa imeshtadi.

Kwa mujibu wa Katiba mpya, lugha 13 za kitaifa zinazozungumzwa nchini humo zimepandishwa hadhi na kuanzia sasa zitatambulika kama lugha rasmi.

Uhusiano kati ya Ufaransa na Mali umeharibika vibaya tangu jeshi lilipoingia madarakani katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi mwaka 2020. Kutokana na mivutano hiyo, Ufaransa ilitangaza kuwaondoa wanajeshi wake nchini Mali mwezi wa Agosti mwaka jana, na hivyo kumaliza operesheni yake ya kijeshi katika nchi hiyo ya Kiafrika baada ya kuwepo kwa miaka 9 katika kalibu ya kikosi cha kijeshi cha Barkhane.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Mali, Choguel Kokalla Maïga, alifichua katika mahojiano maalumu na televisheni ya Al-Jazeera ya Qatar kuwa Bamako ina taarifa sahihi na ushahidi kwamba baadhi ya magaidi walioko nchini Mali wamekuwa wakiwasiliana na Ufaransa.

Mwishoni mwa mwaka jana pia, Baraza la Kijeshi la Mali lilipiga marufuku nchini humo shughuli zozote za mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanafadhiliwa kifedha na Ufaransa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live