Zaidi ya watu 70 walifariki kufuatia kuporomoka kwa mgodi wa dhahabu magharibi mwa Mali siku ya Ijumaa, kiongozi wa kundi la wachimbaji dhahabu na kiongozi aliyechaguliwa katika eneo hilo wameliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumatano.
"Ilianza kwa kelele nyingi. Ardhi ilianza kutikisika. Kulikuwa na zaidi ya wachimba dhahabu 200 chini. Zoez la utafutaji sasa limekamilika. Tumepata miili 73," kiongozi wa wachimbaji dhahabu wa Kangaba, Oumar Sidibé, ameliambia shirika la habari la AFP. Idadi ya wawahangaimethibitishwa na afisa wa eneo hilo.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne, wizara ya madini ilitaja vifo vya wachimba dhahabu kadhaa, bila kutoa takwimu sahihi. Serikali imetoa "rambirambi zake za kusikitisha zaidi kwa familia zinazoomboleza vifo vya ndugu zao na kwa wananchi wa Mali".
Serikali ya Mali imetoa wito kwa "jamii zinazoishi karibu na maeneo ya uchimbaji madini na wachimbadhahabu kuheshimu kwa uangalifu sheria za usalama na kufanya kazi tu katika maeneo
yaliyotengwa kwa uchimbaji wa dhahabu".
Mali, miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa dhahabu barani Afrika.
Maeneo ya kuchimba dhahabu mara kwa mara yanakabiliwa na maporomoko mabaya ya udongo, shughuli hiyo ikiwa hatari na mamlaka inajitahidi kudhibiti uchimbaji wa madini hayo.
Kwa tani 72.2 zilizozalishwa mwaka 2022 (ikiwa ni pamoja na tani 6 kwa uchenjuaji dhahabu), dhahabu pekee ilichangia 25% ya bajeti ya kitaifa, 75% ya mapato ya nje na 10% ya Pato la Taifa, Waziri wa Madini wa wakati huo, Lamine Seydou Traoré alisema mwezi Machi 2023.