Kaimu Waziri Mkuu wa Mali amesema Russia inaliheshimu na imelisaidia pakubwa taifa hilo la Afrika Magharibi katika vita dhidi ya ugaidi, na imethibitisha kivitendo kuwa haina masharti wala malengo fiche kwenye usaidizi wake.
Choguel Kokalla Maiga amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la RIA Novosti na kueleza kuwa, kwa msaada kijeshi wa Russia, hivi magaidi hawawashtui tena wananchi wa Mali, bali magenge ya kigaidi yanatiwe kiwewe hivi sasa na jeshi la nchi hiyo.
Maiga ameeleza bayana kuwa, Russia ni rafiki na mshirika wa kutegemea kwa Mali na mataifa mengine ya Afrika, na wala haina undumakuwili na nyuso mbili kwenye misimamo na sera zake.
Kaimu Waziri Mkuu wa Mali amesema misaada ya Russia kwa taifa hilo haishii tu kwenye silaha za zana za kijeshi, lakini pia katika masuala ya kibinadamu kama misaada ya chakula, mbolea, na nishati.
Maiga amesema, "Hatutaki kuwa mateka wa mataifa mengine, ambayo mpaka yafanye maamuzi ya kutupa au kutotupa fueli na kuweka chakula kwenye meza ya wananchi wa Mali."