Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malawi yatupilia mbali mashtaka dhidi ya mkuu wa kitengo cha kupambana na ufisadi

B423c395 0ad4 40b7 B8bf 2cc168132ebe Malawi yatupilia mbali mashtaka dhidi ya mkuu wa kitengo cha kupambana na ufisadi

Mon, 13 Feb 2023 Chanzo: Bbc

Malawi imetupilia mbali mashtaka ya jinai dhidi ya mkuu wa shirika la kupambana na rushwa kufuatia shinikizo kutoka kwa wafadhili wakuu wa nchi hiyo na mashirika ya kiraia.

Martha Chizuma alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kashfa ya jinai kutokana na sauti iliyovuja ambapo alidaiwa kutoa matamshi yanayoashiria kuwa baadhi ya maafisa wakuu serikalini na baadhi ya maafisa wa mahakama wanazuia vita dhidi ya ufisadi.

Katika taarifa yake mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alisema alikomesha kesi hizo kufuatia uhakiki na mashauriano na mwanasheria mkuu wa serikali.

"Niliamua kusitisha kesi ya jinai dhidi ya Bi Chizuma kulingana na maagizo ya katiba na sheria zingine zinazohusika," Masauko Chamkakala alisema.

Lakini wakili wa Bi Chizuma aliambia shirika la VOA kwamba mashtaka hayajafutwa rasmi.

Matamshi hayo yanayodaiwa kuwa ya kashfa yamo katika mazungumzo ya faragha yaliyorekodiwa kwa siri ambayo Bi Chizuma alikuwa nayo na mtu asiyeajiriwa na ofisi yake.

Kesi hizo zilimfanya kusimamishwa kazi kabla ya kurejeshwa ofisini wiki jana na mahakama kuu.

Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya wote walikuwa wametoa taarifa wakieleza "wasiwasi wake mkubwa" juu ya kusimamishwa kwake kazi.

Chanzo: Bbc