Waziri wa Elimu nchini Malawi, Agnes Nyalonje amezindua darasa la kwanza la lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Hebron.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Nyalonje alisema uanzishwaji wa darasa hilo ni kati ya ushirikiano wa Tanzania na Malawi.
“Ushirikiano huu ni muhimu na wenye thamani, tutauenzi na kuhakikisha Kiswahili kinakua kwa kasi nchini kwetu,” amesema.
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Humphrey Polepole amesema uanzishwaji wa darasa hilo ni muendelezo wa uhusiano mzuri wa nchi hizo na kwamba atasimamia utekelezaji katika kuhakikisha Kiswahili kinakua.
Polepole alisema huu ni mwanzo na serikali ina imani na uhusiano huo wa vyuo utazidi na kuimarisha uhusiano mzuri katika nchi zote.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo aliishukuru Serikali ya Malawi kwa kukubali kuanzisha ushirikiano huo na kuwa lugha ya Kiswahili itakuwa zaidi kutokana na uanzishwaji wa darasa.
Nombo alisema anaamini watu wengi wa Malawi wataweza kuelewa haraka lugha ya Kiswahili ambayo itawasaidia katika nyanja mbalimbali.
Darasa hilo la kwanza lilizinduliwa Novemba 10 nchini Malawi katika Chuo Kikuu cha Hebron ambapo walimu wa darasa hilo wanaofundisha kwa muda wa wiki moja wametoka katika Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).