Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makumi ya watu wauawa katika mashambulizi ya 'kinyama' Burkina Faso

Makumi Ya Watu Wauawa Katika Mashambulizi Ya 'kinyama' Burkina Faso Makumi ya watu wauawa katika mashambulizi ya 'kinyama' Burkina Faso

Sun, 9 Apr 2023 Chanzo: Bbc

Takriban watu 44 wameuawa baada ya mashambulizi mawili mabaya kaskazini mwa Burkina Faso siku ya Alhamisi, maafisa wamesema.

Mashambulizi hayo mawili yalitokea katika vijiji vya Kourakou na Tondobi katika eneo la Sahel, karibu na mpaka wa Niger.

Hakuna kundi lililokiri kufanya mashambulizi hayo, lakini ghasia za wanajihadi ni za kawaida katika eneo hilo na maafisa wamelaumu "makundi ya kigaidi yenye silaha".

Makundi ya wapiganaji wanaohusishwa na al-Qaeda na Islamic State (IS) yanajulikana kufanya kazi katika eneo hilo.

Luteni-Gavana wa eneo la Sahel, Rodolphe Sorgho, alisema washambuliaji waliendesha "shambulio la kuchukiza na la kinyama".

Wanakijiji wengine waliripotiwa kujeruhiwa katika mashambulizi hayo, lakini haijulikani ni wangapi. Bw Sorgho alisema "hatua za kuleta utulivu eneo hilo zinaendelea".

Mkazi mmoja aliliambia shirika la habari la AFP kwamba "idadi kubwa ya magaidi waliingia kijijini" na kwamba alisikia milio ya risasi usiku kucha.

"Ilikuwa Ijumaa asubuhi ambapo tuliona kwamba kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa wamefariki dunia," alisema.

AFP pia imeripoti kwamba mauaji hayo yalikuwa ya kulipiza kisasi kwa wanajihadi wawili ambao walijaribu kuiba ng'ombe siku chache zilizopita.

Mauaji ya Alhamisi usiku yalitokea karibu na kijiji cha Seytenga, ambapo makumi ya watu waliuawa Juni mwaka jana.

Burkina Faso na majirani zake wamekabiliwa na uasi wa muda mrefu wa wanajihadi tangu 2013.

Maelfu ya watu wameuawa wakati wa mzozo huo na zaidi ya milioni mbili wametoroka makazi yao.

Ghasia hizo zimesababisha msukosuko mkubwa wa kisiasa nchini humo.

Jeshi - likiongozwa na Lt Kanali Paul-Henri Damiba - lilichukua mamlaka nchini humo Januari mwaka jana, na kuahidi kukomesha ghasia.

Lakini alishindwa kukomesha mashambulizi, na aliondolewa katika mapinduzi ya pili na Kapteni Ibrahim Traoré Septemba iliyofuata.

Capt Traoré ameahidi kushinda tena eneo kutoka kwa wanajihadi, na kufanya uchaguzi wa kidemokrasia mnamo Julai 2024.

Mkuu wake mpya wa kijeshi, Kanali Celestin Simpore, aliapa mapema wiki hii kuongeza "uvamizi mkali" ili kukabiliana na wanajihadi.

Lakini Kapteni Traoré pia amewataka wanajeshi wa Ufaransa kuondoka nchini humo na kumekuwa na uvumi mkubwa kwamba huenda akaanza kufanya kazi na mamluki wa Urusi.

Chanzo: Bbc