Mwanafunzi mmoja amefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya bomu kulipuka katika eneo la Kaskazini-Magharibi la Cameroon.
Tukio hilo lilitokea Jumapili wakati wanafunzi hao wakiandamana kuadhimisha siku ya vijana nchini katika mji wa Nkambe.
Video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha wanafunzi wakikimbilia usalama baada ya mlipuko huo.
Mkuu wa mkoa aliviambia vyombo vya habari vya serikali kuwa mwanafunzi mmoja aliuawa na watu 40 walijeruhiwa katika tukio hilo.
Gavana Adolphe Lele L'Afrique alisema wapiganaji wanaotaka kujitenga wanashukiwa kufanya shambulio hilo.
Wapiganaji hao wa Anglophone walikuwa wameweka kizuizi ili kutatiza sherehe hizo.
Mashambulizi dhidi ya wanafunzi, walimu na taasisi za elimu ni ya kawaida katika eneo la Cameroon ambalo wakazi wake wanazungumza lugha ya Kiingereza.
Tukio hilo linaonekana kama jaribio la wapiganaji hao kutekeleza mgomo wao dhidi ya elimu, ambayo waliiweka zaidi ya miaka saba iliyopita.