Makanisa na misikiti katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, yamehimizwa "kuzingatia" na kupunguza viwango vya juu vya kelele katika majengo yao.
Katika ujumbe wake wa Twitter, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alisema atakuwa na majadiliano na viongozi wa kidini kuhusu kudhibiti viwango vya sauti.
Hivi majuzi jiji hilo lilipiga marufuku vilabu vya usiku kuhudumu katika maeneo ya makazi kufuatia malalamiko kutoka kwa wakaazi kuhusu kelele huku wakazi wengi wakitoa wito wa kupigwa marufuku kwa sehemu kama hizo za ibada - zinazojulikana kwa kuwa na mifumo ya muziki ya kelele.
Bw Sakaja alisema: "Hata na vilabu vya usiku; hatukuanza kwa kuvifunga. Tulizungumza nao baada ya muda, walikubali kufuata lakini wengine walipuuza. Kisha tukachukua hatua."
Mapema Alhamisi, gavana huyo alisema hatafunga sehemu za ibada lakini badala yake ataanzisha mazungumzo.
Nairobi ina idadi kubwa ya makanisa ya kiinjili ambapo muziki wa sauti ya juu ni kawaida wakati wa ibada na mikesha ya usiku kucha.